Habari za hivi Punde

HUHESO YATOA ELIMU KWA MADREVA MATUMIZI SAHIHI YA CONDOM




SHIRIKA la The Foundation for Human Health Society [HUHESO FOUNDATION] lenye makao makuu yake mjini Kahama limetoa elimu kwa wanaume wanaofanya kazi kwenye malori,migodini na madreva wa bodaboda juu ya matumizi sahihi ya Kondomu.

Mafunzo hayo yalitolewa na Shirika hilo baada ya kubaini chanzo kikubwa cha wanawake kufanya mapenzi yasiyo salama ni wanaume ambao wengi wao hufikia nyakati za matamanio kwenye mazingira ya starehe.


 Mkurugenzi wa Shirika hilo Juma Mwesigwa katika mafunzo hayo alisema idadi kubwa ya wanaume hao huwachukua wanawake usiku wa manane baadhi yao wakiwa katika ulevi hali ambayo hujikuta wakiwaingilia wanawake pasipo Kondomu.

 Mwesigwa alisema uchunguzi wa Shirika lake umebaini wengi wa wanaume wakiwa kwenye starehe huchukua wanawake bila maandalizi wakati mwingine mida ambayo maduka ya kuuza kondomu yamefungwa hivyo kuwa chanzo cha kufanya ngono isiyo salama.

Kufuatia hali hiyo Shirika la HUHESO Foundation limeelekeza nguvu ya mafunzo kwa wanaume baada ya kutoa elimu hiyo kwa wanawake ambao wengi wao walilalamika kitendo cha wanaume hao kuwaingiza kwenye nyumba za kulala wageni bila kuwa na kondomu.

Walidai kitendo hicho huwafanya waingiliwe bila kinga hiyo kwakuwa wanaume hao huwatishia maisha kutokana na gharama walizozitumia kwenye starehe kuwa kubwa hivyo kuwalazimisha kufanya mapenzi bila kondomu baada ya kukosa pa kuzipata kutokana na kuwa usiku wa manane.

Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo na Uelimishaji wa Shirika la HUHESO;Ali Lityawi alisema wameamua kutoa mafunzo katika kundi hilo ikiwa ndilo kundi kubwa lenye muingiliano mkubwa wa watu kutokana na shughuli zao kuwa nje ya familia zao.

Lityawi alisema lengo la mafunzo hayo ambayo ni utekelezaji wa Mradi wa kuwakomboa wanawake na wasichana wanaoishi katika mazingira magumu na kufanya biashara ya ngono unaofadhiliwa na Rapid Fund Envelope {RFE} ni kuwafikia wanawake na wanaume elfu Tatu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

0 Response to "HUHESO YATOA ELIMU KWA MADREVA MATUMIZI SAHIHI YA CONDOM"

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.