Habari za hivi Punde

UKOSEFU WA MITANDAO YA MAJI SAFI NA SALAMA HUFANYA BAADHI YA MAENEO KUKOSA MAJI.





UKOSEFU  wa mitandao ya maji safi na salama katika baadhi ya maeneo ya Shinyanga mjini ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (SHUWASA )  hali ambayo inasababisha baadhi ya maeneo kukosa huduma muhimu ya maji.

 Hayo yamebainishwa na mkurugenzi mtendaji wa SHUWASA injinia Silvester Mahole wakati akisoma taarifa kwa mgeni rasmi ambaye alikuwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi kwenye uzinduzi wa mradi wa maji kutoka ziwa Victoria katika kijiji cha Ibadakuli katika manispaa ya Shinyanga .


 Mahole alisema mahitaji halisi ya maji kwa wakazi wa Shinyanga mjini ni milimita za ujazo 16,969 lakini wamekuwa wakilazimika kuzalisha maji yenye milimita za ujazo 7000 hadi 8000 kutoka kwenye tenki la maji lililopo  eneo la Old Shinyanga kutokana na kukosekana kwa mitandao ya maji hivyo kufanya matumizi ya maji kuwa machache.

 Alisema  kuwa licha ya SHUWASA kuwa na uwezo wa kuzalisha maji hayo kwa asilimia 100 kutoka katika vyanzo vyake vya maji kama vile mradi wa ziwa Victoria pamoja na Bwawa la Ning’hwa lililopo katika wilaya ya Shinyanga lakini hadi sasa kiwango cha utoaji huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa mjini Shinyanga ni asilimia 58.5.

“Sababu ya kutozalisha maji hayo kwa asilimia 100 kwa wakazi wa mjini Shinyanga ni kutokana na mtandao uliojengwa chini ya mpango wa maendeleo ya sekta ya maji nchini mjini hapa kwa awamu ya kwanza (Water Sector Development) haukuweza kufika katika baadhi ya  makazi” alisema Mahole.

Akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama katika kijiji hicho cha Ibadakuli Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi ambaye alikuwa mgeni Rasmi kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga alisema mwaka 2007 hadi 2009 mji huo ulibahatika kupata mradi wa maji  lakini kutokana na ufinyu wa bajeti  baadhi ya maeneo  miundombinu haikumalizika kujengwa

Nyamubi alifafanua kuwa kutokana na kutopatikana kwa fedha yote waliyokuwa wameahidiwa na washirika wa maendeleo (Development Partners) alisema  asilimia 50 ya fedha hizo zilitekelezwa kwa ujenzi wa miundombinu ya maji katika baadhi ya maeneo huku maeneo mengine yakikosa.

Nyamubi aliyataja baadhi ya maeneo ya mjini Shinyanga ambayo hajafikiwa na huduma ya maji  safi na salama kutokana na ukosefu wa mitandao ya kusambaziwa maji kutoka ziwa Victoria eneo la  Ngokolo, Mwawaza, Kizumbi,Bugweto, Chibe,Bushushu pamoja na Kolandoto.

0 Response to "UKOSEFU WA MITANDAO YA MAJI SAFI NA SALAMA HUFANYA BAADHI YA MAENEO KUKOSA MAJI."

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.