Habari za hivi Punde

HALMASHAURI WILAYA YA KISHAPU IMEBAINI KAYA 5881 KUKOSA VYOO




HALMASHAURI ya  wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga imebaini kaya  5881 kutokuwa na vyoo ikiwa kaya  3335 zimejenga vyoo vya muda  hali ambayo  inaonyesha kuwa  hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko hasa ya  kuhara na kipindupindu.

Kaya hizo zilibainika wakati  wa kampeni  inayoendelea ya usafi wa mazingira na kuihamasisha jamii kuwa na vyoo bora katika kata zote za wilaya hiyo  kwa kutumia sheria ndogo za halmashauri, huku mila na desturi  zikitajwa kuwa ni chanzo cha kuwepo tatizo hilo  na kuona ni muhimu kwa kujisaidia vichakani.

Akizungumza na waandishi wa habari afisa mazingira wa wilaya ya Kishapu Mohamed Mlewa, alisema wilaya inakaya 42,000 kati ya hizo zenye vyoo bora ni 12,680 vya kawaida 20,114 na ambavyo  vimejengwa kwa matumizi ya muda ni 3335 huku kaya 5881 vikiwa havina vyoo .

“Ni muhimu kila kaya iwe na choo tena tunasisitiza kiwe bora na ndiyo maana tunaendelea kutoa elimu kwa jamii, iweze kubadilika iache mila na desturi zilizopitwa na wakati kama sasa hivi  tumebaini kuwepo kaya 5881 zisizokuwa na vyoo  hata vya muda hawana”alisema Mlewa.

Alisema walitembelea kata za Masanga ,Shagihilu,Mwamashele na Ukenyenge  ambapo walizungumza na wananchi na kutoa elimu sanjari na kukagua kaya  kama zinavyoo nakukuta baadhi hazina ambazo walizitaka kuhakikisha wanachimba haraka il kuzuia kuibuka magonjwa ya mlipuko.

Ameitaka  jamii kubadilika kwa kuhakikisha mazingira wanayoishi yanakuwa safi ,hatua itakayosaidia kujiepusha kukumbwa  na kipindupindu hasa kipindi hiki cha mvua za masika zinazoendelea kunyesha, ambapo hutokea mlipuko wa magonjwa mbalimbali mazingira yakiwa machafu.

Wakati huo huo ilibainika pia  kukosekana  kwa miundombinu bora ya maji na vyoo pamoja na mazingira machafu umesababisha nyumba za kulala wageni tatu na hoteli mbili kufungwa, katika halmashauri  hiyo.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya idara  ya usafi wa mazingira wilayani humo kufanya ukaguzi na kubaini kuwepo changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa maji,kalo la maji machafu na miundombinu ya ndani kutoridhisha yakiwemo mashuka hivyo kuhatarisha afya za wateja.

.“Hili zoezi lilifanyika march 27 mwaka huu katika mji wa mhunze ambapo tulifunga hotel  mbili na kisha mji mdogo wa Maganzo hoteli moja na nyumba za kulala wageni mbili,tunaendelea na zoezi hili kwa wilaya nzima ili kuhakikisha mazingira yote yanakuwa safi ”alisema Mlewa.

Afisa mazingira alisema zoezi hilo limeanza kwa kupitia hoteli na baa na kwamba hatua itakayofuata ni kukagua migahawa,ambapo aliwataka  wananchi kuhakikisha wanaweka mazingira katika hali ya usafi ili kuzuia mlipuko wa magonjwa ambao unaweza kutokea kwa kusababishwa na uchafu.

0 Response to "HALMASHAURI WILAYA YA KISHAPU IMEBAINI KAYA 5881 KUKOSA VYOO"

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.