SHIRIKA la The Foundation for Human Health Society [HUHESO
FOUNDATION] lenye makao makuu yake mjini Kahama limetoa elimu kwa wanaume
wanaofanya kazi kwenye malori,migodini na madreva wa bodaboda juu ya matumizi
sahihi ya Kondomu.
Mafunzo hayo yalitolewa na Shirika hilo baada ya kubaini
chanzo kikubwa cha wanawake kufanya mapenzi yasiyo salama ni wanaume ambao
wengi wao hufikia nyakati za matamanio kwenye mazingira ya starehe.
Mkurugenzi wa Shirika hilo Juma Mwesigwa katika
mafunzo hayo alisema idadi kubwa ya wanaume hao huwachukua wanawake usiku wa
manane baadhi yao wakiwa katika ulevi hali ambayo hujikuta wakiwaingilia
wanawake pasipo Kondomu.
Mwesigwa alisema uchunguzi wa Shirika lake umebaini
wengi wa wanaume wakiwa kwenye starehe huchukua wanawake bila maandalizi wakati
mwingine mida ambayo maduka ya kuuza kondomu yamefungwa hivyo kuwa chanzo cha
kufanya ngono isiyo salama.
Kufuatia hali hiyo Shirika la HUHESO Foundation limeelekeza
nguvu ya mafunzo kwa wanaume baada ya kutoa elimu hiyo kwa wanawake ambao wengi
wao walilalamika kitendo cha wanaume hao kuwaingiza kwenye nyumba za kulala
wageni bila kuwa na kondomu.
Walidai kitendo hicho huwafanya waingiliwe bila kinga hiyo
kwakuwa wanaume hao huwatishia maisha kutokana na gharama walizozitumia kwenye
starehe kuwa kubwa hivyo kuwalazimisha kufanya mapenzi bila kondomu baada ya
kukosa pa kuzipata kutokana na kuwa usiku wa manane.
Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo na Uelimishaji wa Shirika
la HUHESO;Ali Lityawi alisema wameamua kutoa mafunzo katika kundi hilo ikiwa
ndilo kundi kubwa lenye muingiliano mkubwa wa watu kutokana na shughuli zao
kuwa nje ya familia zao.
Lityawi alisema lengo la mafunzo hayo ambayo ni utekelezaji
wa Mradi wa kuwakomboa wanawake na wasichana wanaoishi katika mazingira magumu
na kufanya biashara ya ngono unaofadhiliwa na Rapid Fund Envelope {RFE} ni
kuwafikia wanawake na wanaume elfu Tatu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
0 Response to "HUHESO YATOA ELIMU KWA MADREVA MATUMIZI SAHIHI YA CONDOM"
Post a Comment