Habari za hivi Punde

SHULE INACHANGAMOTO NYINGI WALIMU WALALA MADARASANI,SHULE HAINA VYOO WALA MADAWATI





SHULE  ya msingi Mwamashimba  katika kijiji  hicho  kata ya Mwamalasa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyoo,madawati na nyumba za walimu hali inayosababisha baadhi ya walimu kuishi kwenye vyumba vya madarasa.

Shule hiyo yenye muonekano tofauti  na kuwa hali halisi ya kuwepo kwa wanafunzi na walimu   waandishi wa habari  walitembelea shule hiyo  kutaka kufahamu  wanafunzi wanapataje elimu kupitia vyumba hivyo na mazingira yaliyopo huku wakihoji baadhi ya viongozi.


Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Mwashimba Elias Zengo alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1976 ina jumla ya wanafunzi 492 na walimu tisa pekee wa kiume 8 na mwalimu wa kike mmoja.

Alisema  changamoto  inayoikabili shule hiyo ni upungufu wa vyumba vya madarasa, ukosefu wa vyoo vya wanafunzi , nyumba za walimu kwani zilizopo sasa ni nyumba mbili pekee hali inayowafanya baadhi ya walimu kuishi kwenye vyumba vya madarasa.

Shule hii inakabiliwa na ukosefu wa  vyoo vya  wanafunzi hali inayowafanya wanafunzi kutumia choo ambacho hakijakamilika baada ya ujenzi wake kukwama na kuongeza kuwa pia upungufu wa madawati unasababisha baadhi ya wanafunzi kukaa chini na uhaba wa nyumba za walimu  unaowafanya  kuishi kwenye madarasa”alisema  mwalimu Zengo.

Kwa upande wake afisa mtendaji wa kijiji cha Mwamashimba Julius Emanuel  ilipo shule hiyo alikiri kuwepo kwa changamoto hizo na kuongeza kuwa wanajiandaa kufanya mkutano na wananchi ili kuangalia namna ya kuzitatua hizo kama vile kuchanga pesa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu.

“Mara nyingi,wananchi wa kijiji hiki wamekuwa mstari wa mbele kuchangia miradi ya maendeleo,hata ujenzi wa choo ambacho hakijakamilika umetokana na nguvu zao,na ujenzi ukifikia usawa wa renta ndiyo huwa tunaomba msaada kutoka serikalini”,alisema afisa Mtendaji.

Naye diwani wa kata ya Mwamalasa ilipo shule hiyo ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu Justine Sheka alisema suala la walimu kuishi kwenye vyumba vya madarasa linatokana na shule hiyo kutokuwa na wanafunzi wa kutosha na kutokana na upungufu wa nyumba za walimu.

“Shule hii ni kongwe imejengwa mwaka 1976,nimekuwa  diwani wa kata hii kupitia CCM tangu mwaka  1994, shule ilikuwa na madarasa ya tope ,tukajenga mapya ,wanafunzi wakawa wachache,na kwa sababu ya upungufu wa nyumba za walimu tukatumia busara kuyageuza  baadhi ya madarasa kuwa nyumba za walimu”alisema Sheka.

 Sheka alisema tayari jumla ya shilingi  milioni 9 zimetengwa  na halmashauri ya wilaya ya Kishapu kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika shule hiyo na shilingi milioni 30 kwa ajili ya madawati katika shule za msingi wilayani humo ikiwemo shule ya msingi Mwamashimba.

0 Response to " SHULE INACHANGAMOTO NYINGI WALIMU WALALA MADARASANI,SHULE HAINA VYOO WALA MADAWATI"

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.