WAZAZI na walezi waliopeleka watoto wao katika
kituo maalumu cha kulelea watoto wenye ulemavu
mbalimbali kilichopo Buhangija manispaa ya Shinyanga wameombwa kujenga
desturi ya kuwatembelea watoto hao mara kwa mara na sio kukiachia
kituo pekee hali ambayo inawafanya kukosa haki zao za msingi
kwa kupata malezi bora kama watoto wengine.
Baadhi ya watoto hao tangu waletwe kituoni hapo hakuna
hata mzazi au mlezi mmoja aliyekuja katika kituo hicho kumuona mwanaye na
kumjulia hali jambo ambalo linaonywesha kuwa watoto tayari wamekosa imani
na wazazi wao kwa kutowaona muda mrefu.
Hali hiyo ilijionyesha wakati familia ya
Mwalongo ilipokwenda kutoa msaada wa vyakula mbalimbali
kwaajili ya kusherekea sikukuu ya pasaka ikiwemo mbuzi
wanne,kilo mia moja za mchele na lita 20 za mafuta ya kupikia vyenye
thamani ya zaidi ya shilingi laki tatu na kuvigawa katika
kambi za kituo cha Buhangija na kituo cha Kolandoto cha kulelea wazee
wenye ukoma ikiwa ilibainika kuwa idadi kubwa ya
watoto wenye ulemavu wa ngozi kutokwenda makwao kutokana na hofu ya
kuuwawa.
Mlezi wa kituo hicho Maisala Adinani alisema
kuwa hali iliyopo kweli baadhi ya wazazi au walezi wamekuwa wakishindwa
kuja kuwaona watoto wao kuna wengine tangu waletwe imefika miaka saba
hawajawahi kuwaona wazazi wao ama kuwatembelea na kuwajulia hali.
Ikiwa imeelezwa kuwa idadi ya watoto
walipo ni 258 kati ya hao wenye ulemavu wa ngozi (Albino) ni 172,wasioona 48 na
viziwi ni 38 ambapo kila baada ya wiki moja mtoto
analetwa ndani ya kituo hicho na wazazi kutofika ili kuwajulia hali hata
kipindi hiki cha siku kuu ya pasaka.
Naye katibu wa chama cha wasioona manispaa ya
Shinyanga Richard Mpongo alisema kuwa tabia ya wazazi
kuwatelekeza watoto katika kituo hicho sio jambo la hekima huko ni kuwanyima
haki zao za msingi kama wazazi na kufanya watoto hao kukosa upendo,hivyo jamii
imetakiwa kuondoa dhana ya mauaji na kuwatenga walemavu huku
wakiwafanya kusihi maisha ya mashaka na hofu kubwa.
Mmoja wa wanafamilia hiyo Anna Mwalongo alisema kuwa
wameguswa na kundi hilo lisilojiweza kwani jamii imekuwa ikiwatenga na
kuwauwa hivyo serikali inatakiwa kukemea kwa nguvu zote ,pia wazazi
wao wasiwatelekeze wawaone kuwa na umuhimu kama watoto wengine
ikiwa wamekuwa wakikosa mambo ya msingi kwa wazazi ikiwemo upendo.
0 Response to "WAZAZI NA WALEZI WALAUMIWA KUWATELEKEZA WATOTO WAO KATIKA KITUO CHA KULELEA WATOTO WALEMAVU"
Post a Comment