Habari za hivi Punde

SERIKALI IMEANZA KUTEKELEZA KUONDOA KERO YA MAJI WILAYANI KISHAPU




WAKAZI wa  wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wameanza kutekelezewa  na serikali  tatizo  la ukosefu wa maji  la muda mrefu  kwa kuanza na usanifu wa njia za upatikanaji wa maji  safi na salama  kutoka ziwa victoria  kama maeneo mengine ndani ya mkoa huu yanavyopata maji.

Hayo yalisemwa na waziri  wa maji  Jumanne Maghembe kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya mji mdogo wa maganzo uliohudhuriwa na  baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo huku akisema kuwa  lazima kero hiyo itatuliwe na kufikia mwaka 2015 asilimia 75 wawe wanapata maji.


Maghembe aliwaeleza wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa tatizo la maji kwa wilaya hiyo lazima liondoke ,kwani kazi ya usanifu njia ya upatikanaji  wa maji  ya ziwa victoria  ufanyike haraka gharama zake zipelekwe wizarani  mwisho mwezi Mei mwaka huu ikiwa bajeti tayari ilikwisha tengwa.

“Tatizo hili lazima tulitatue  katika kutafuta ufumbuzi ambapo viongozi ndani ya mkoa huu wamekuwa wakipiga hodi sehemu mbalimbali ili kuweza kukopa fedha  za kuondoa kero ya maji, katika utekelezaji wa  mradi wa  maji vijijini ,kwa wilaya hii imepiga hatua kubwa  nzuri mwaka jana kwa Tanzania nzima  kutekeleza mradi kwenye vijiji 10 vikiwemo mwigumbi na mwamashimba ambao kwa sasa wanapata maji.”alisema Maghembe.

Naye  Mbunge wa jimbo hilo  Selemani Nchambi alisema kuwa kuanzia kata ya Songwa mpaka Mhunze wanatatizo kubwa  la upatikanaji wa maji  ikiwa ahadi aliyokuwa akiitoa kipindi cha kampeni  kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2010 ni kuwapatia maji safi na salama  ambapo ni vijiji viwili vya Mwigumbi na Mwamashimba vimetekelezewa  mradi wa kuchimbiwa visima virefu na ndio wanapata maji safi na salama. 

Mkuu wa mkoa  Ally Rufunga alisema kuwa kumekuwepo na tatizo la maji  hasa kwa wakazi wa mji mdogo wa Maganzo  hivyo kero hiyo sasa inashughulikiwa na kuisha ikiwa tayari waziri mwenye dhamana  yuko mbele ya wananchi wa wilaya hii kwa kujionea hali halisi ilivyo ambapo  serikali ya mkoa nayo imefanya jitihada ya kupata fedha na kutekeleza kauli mbiu ya kila  wilaya kwa mwaka kuwepo na utekelezaji wa mradi wa maji katika  vijiji kumi. 

Mkazi wa kijiji cha Lubaga  Sesilia John  alisema  wanawake wengi wa Kishapu wanavunja miji yao  kutokana na shida ya maji ambapo hulazimika kuwaacha wanaumme wao kila siku saa 11 alfajiri  hali inayosababisha wanaumme hao kuvunja kwa ndoa au kutafuta mwanamke mwingine.

“Wanwake wa kishapu pia wanabakwa,kupigwa na hata kuvamiwa na wanyama aina ya fisi pindi wanapofuata huduma ya maji nyakati za usiku,mfano katika vijiji vya  Lubaga na Isoso   kuna tatizo la  maji  hata kufa kwa mifugo yetu”,  alisema Sesilia.


0 Response to "SERIKALI IMEANZA KUTEKELEZA KUONDOA KERO YA MAJI WILAYANI KISHAPU"

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.