Habari za hivi Punde

MRADI WA GESI WA MTWARA UNATARAJIA KUANZA MAJARIBIO JIJINI DAR.


Na Anitha Jonas, MAELEZO-DSM
SERIKALI imesema kuwa mradi wa gasi kutoka Mtwara hadi katika kituo cha Kinyerezi jijini Dar es Salaam unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwaka huu (2014) na kuanza majaribio Januari, 2015.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw. Eliakim Maswi wakati wa ziara ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mitambo ya gesi katika eneo la Kinyerezi.
Katibu Mkuu huyo alisema hadi hivi sasa mradi huo wa gesi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 70.(Martha Magessa)
Aliongeza kuwa hivi sasa uzalishaji wa umeme katika Shirika la TANESCO unaigharimu Serikali shilingi1.6 trilioni kwa mwaka, hivyo baada ya mradi huo kukamilika, serikali itaokoa kiasi hicho cha fedha na kuzielekeza katika miradi mingine ya jamii.
Mradi wa gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam utagharimu dola za Kimarekani shilingi 183 millioni, hadi sasa, serikali imekwishalipa Dola milioni 139 bado dola 44 millioni.
Naye Mhandisi wa mradi huo Bw. Simon Gilima, alisema kuwa jumla ya Megawatt 150 zitazalishwa na kuingizwa kwenye gridi ya taifa na kusaidia uzalishaji wa umeme kwa bei nafuu.
Mmoja wa wadau wa maendeleo nchini ambaye pia ni Mkurugenzi wa UN nchini Bw. Philippe Dongier alielezea kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ambao pia alisema utaongeza ajira nchini na pato la taifa.
Aliishauri Seriakli ya Tanzania kuendelea kubuni miradi mingine itakayosaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.
Vile vile aliiomba Serikali kuwa makini na masuala ya uwekezaji ili kulinda na kusimamia Sera na matakwa ya nchi.
Ziara hiyo ya Katibu Mkuu huyo kwenye eneo hilo ililenga kuangalia maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ambapo pia iliwashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo nchini ikiwemo Benki ya Dunia, JICA, Umoja wa Mataifa (UN) na TPDC.

0 Response to "MRADI WA GESI WA MTWARA UNATARAJIA KUANZA MAJARIBIO JIJINI DAR."

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.