Habari za hivi Punde

MKUU WA MKOA WA SHINYANGA AZINDUA MRADI WA MAJI KATIKA KIJIJI CHA BUBINZA.



SERIKALI mkoani Shinyanga imezindua  mradi wa maji katika kijiji cha Bubinza kata ya mwamashele wilayani Kishapu  ambao utaondoa changamoto  kwa wananchi wa kijiji hicho ambapo walikuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali yakiwemo magonjwa ya mlipuko  kutokana na kutumia maji yasiyo salama.

Akizindua mradi huo  mkuu  wa mkoa  Ally  Rufunga alisema lengo la serikali hapa nchini hadi kufikia 2025 ni kuhakikisha vijiji vyote vinaondokana  na matatizo ya maji safi na salama hali ambayo itaimarisha uchumi wa nchi kutokana na asilimia kubwa ya wananchi kutumia muda  wa kutafuta maji  badala yake watafanya  shughuli za kimaendeleo.


Rufunga alisema tatizo la maji hapa nchini huathili shughuli za kiuchumi kutokana na wananchi wanaopatwa na adha hiyo kutumia muda mwingi kutafuta maji hayo, huku wengine wakitumia muda huo kupata tiba za afya zao sababu ya kutumia maji ambayo siyo salama.

Alisema katika mwaka huu wa fedha 2013/14 serikali katika mkoa wa shinyanga hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu mkoa umeshapokea fedha shilingi Bilioni 2.5 kutoka serikali kuu fedha ambazo zitatekeleza miradi ya maji katika vijiji vya mkoa huu.

Akisoma taarifa ya mradi wa maji kwa mgeni Rasmi kaimu afisa mtendaji wa kijiji hicho Luhende Njungu, alisema mradi huo ulivumbuliwa na wananchi wenyewe mwaka 2009 ambapo ujenzi wake ulianza  mwezi septemba mwaka jana na kutarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi march 2014 ambao utaghalimu  kiasi cha shilingi millioni 500.

Njungu alisema kutokana na sera ya maji ya mwaka 2002 kijiji kilipaswa kuchangia fedha kiasi kwa kusaidiana na serikali ambapo kijiji hicho kilichangia shilingi milioni 12.5 na fedha zilizobaki zilitolewa na serikali kwa ajili ya kukamilisha mradi huo ambao utasaidia kutatua kero ya maji kwa wanakijiji  zaidi ya  4,800.


Baadhi ya akina  mama wakijiji hicho  ambao ni Stella Idukio na Mhoja John  wakiongeea juu ya matatizo waliyokuwa wanayapata kutokanana na uhaba wa maji safi na salama walisema walikuwa wanagombana na waumezao kutokana na kuamka usiku kwenda kutafuta maji hayo, huku baadhi yao wakivunja miji, na wengine kubakwa.

‘’Tunashukuru serikali kutusaidia kuzindua mradi huu wa maji ambao kwa asilimia kubwa utatusaidia kutatua matatizo yetu hasa sisi akina mama ambao kwa asilimia kubwa ndio watafutaji wa maji haya safi na salama” walisema akina mama hao.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya hiyo ya kishapu Wilison Nkhambaku aliwataka wananchi wilayani humo kutunza miundombinu ya miradi hiyo ya maji ambayo hutumia ghalama kubwa hadi kukamilika kwake hali ambayo itawafanya kusahau matatizo ya maji katika vijiji vya wilaya hiyo ,ambayo ni wilaya kame kuliko wilaya zote mkoani shinyanga.





0 Response to "MKUU WA MKOA WA SHINYANGA AZINDUA MRADI WA MAJI KATIKA KIJIJI CHA BUBINZA."

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.