Habari za hivi Punde

BAADHI YA WANANCHI WA KATA ZA NDALA NA MASEKELO MANISPAA YA SHINYANGA WAILALAMIKIA HOSPITAL YA MKOA KUPANDISHA GHARAMA.


BAADHI ya WANANCHI wa kata za Ndala na Masekelo manispaa ya Shinyanga  wameilalamikia hospitali ya mkoa wa Shinyanga kupatindisha gharama ya kuchukua cheti  cha kuanza matibabu kutoka shilingi 1000 hadi 5000,hali ambayo inasababisha   wenye kipato cha chini kushindwa kupata matibabu  ikichangiwa  kukosekana vituo vya afya na zahanati kwenye maeneo yao.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kata hizo ambazo ziko manispaa ya Shinyanga,walisema gharama imekuwa kubwa ni vema kwanza serikali ingeboresha vituo vya afya  na zahanati na kujenga kila kata, ili kuwasaidia wananchi wenye kipato cha chini kwenda kupata huduma tofauti na ilivyo sasa.

Baadhi ya wananchi hao Hamza Yusufu na Pendo John  kutoka kata ya Masekelo walisema,hospitali ya mkoa haiwezi kupunguza msongamano wa wagonjwa kwa kupandisha gharama ,wakati hakuna huduma kuanzia ngazi za vijiji hadi kata jambo ambalo ni kero kubwa kwa wananchi hasa ambao wanategemea wauuze mazao ndipo wapate kipato.

“Hali inaonekana kuwa mbaya  maana wagonjwa wanashindwa  kutibiwa kwa kuwa  hawana fedha za kulipia cheti cha matibabu ili wakamuone daktari,tunaiomba serikali na uongozi wa hospitali waangalie suala hili kwa umuhimu wake mkubwa maana wanaokwenda kutibiwa hapo siyo wote wanauwezo wengine kupata fedha kiasi hicho ni ngumu"alisema Yusufu.


Mwanahamis Juma mkazi wa ndala alisema hakuna  zahanati wala kituo cha afya kwenye hizo kata mbili zilizojirani, hivyo  wanalazimika kwenda zahanati  ya Kambarage au kituo cha afya  cha kata ya Kambarage,ambako wakati  mwingine dawa hukosekana na kwenda kununua maduka ya madawa.

Kwa upande wake diwani wa viti maalumu kutoka kata hizo Zainabu Kheri alisema ujenzi wa zahanati ukombioni kuanza katika kata ya Masekelo  ili kuwasaidia wananchi kupata huduma kwa ukaribu zaidi tofauti na hivi sasa huduma ziko mbali kwa kata zote mbili.

Akitoa ufafanuzi wa malalamiko hayo ya wananchi mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa  Dkt Fredrick Mlekwa,alisema gharama zilizopo ni za zamani isipokuwa zilizoongezeka ni  gharama ya kuchukua cheti cha matibabu ni shilingi 5000 badala ya 1000,hii inatokana na kwamba kiwango cha 1000 tangu mwaka 1998 imebadilika kutokana na huduma kupanda.

“Awali  mgonjwa akilazwa mwezi mzima alikuwa analipa shilingi 1000 ya kitanda lakini sasa hivi ni 5000 kwa wiki kutokana na gharama za maisha kupanda,vifaa yakiwemo madawa na hivi sasa wananchi wanatakiwa waelewe hii ni hospital ya mkoa ya rufaa kuna gharama zingine zinaongezeka ‘’alisema Dkt. Mlekwa.

Dkt. Mlekwa aliongeza kuwa, hakuna gharama inayotozwa ya kumuona daktari zaidi ya kulipia cheti cha matibabu na kuwataka wananchi kuyaelewa vizuri mabadiliko hayo ya gharama,kwani  kiwango cha shilingi 1000 kimetozwa tangu 1998.

0 Response to "BAADHI YA WANANCHI WA KATA ZA NDALA NA MASEKELO MANISPAA YA SHINYANGA WAILALAMIKIA HOSPITAL YA MKOA KUPANDISHA GHARAMA."

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.