Habari za hivi Punde

WAKAZI WA KIJIJI CHA SANGITA KATA YA USANDA WAKABILIWA NA UHABA WA MAJIBAADHI ya wakazi   wa kijiji cha Singita kata ya Usanda halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa huduma za maji, hali inayowalazimu kwenda kuchota maji mto Shimiwi huku wakihofia afya zao kukumbwa na magonjwa  ya mlipuko  pia kuchangia  na mifugo.

Hayo yalielezwa  na baadhi ya wananchi  wakati wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijijini humo,ambapo walisema hakuna visima vya maji wala  mabomba na kwamba maji wanayotumia wanakwenda kuchimba mtoni na wakati mwingine hukuta fisi wakinywa maji.


Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti  baadhi ya wananchi hao Rehema Samson,Maria Maige na Peter Nkilijiwa,walisema kilio chao wameshakifikisha kwa mbunge wa jimbo  la Solwa  Ahamed Salum na diwani wakata hiyo Abeid Aljabiri lakini bado ufumbuzi haujapatikana.

“Shida ya  maji  ipo hakuna mpaka tufuate mtoni au kununua dumu shilingi 200 na wakati mwingine inafika mpaka 300 kutegemeana na umbali unaokaa,kwa kweli ndugu mwandishi tunateseka tufikishieni kilio chetu kwa serikali tumekuwa kama watoto yatima hatuna msaada”alisema Maria Maige.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji hicho Mohamed Jumanne,alisema kuna vitongoji 10 lakini vyote havina huduma ya maji ya kuridhisha, ambapo ameiomba serikali kusikia kilio chao na kuwapatia msaada wa haraka kwa kuwachimbia visima ili waondokane na kero hiyo.

Mwenyekiti huyo alisema ,hali huwa mbaya zaidi wakati wa kiangazi  kwa kuwa maji  hukauka mtoni, hivyo wananchi huchimba kwa kufuata mkondo wa mto ili wapate maji jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha yao kwa kufukiwa na udongo unaokuwa umerundikwa kwa kuwa wanakuwa ndani ya shimo.

Naye diwani wa kata hiyo Abeid Aljabiri akitoa ufafanuzi wa tatizo hilo alisema,halmashauri ilitoa ahadi ya kuwachimbia visima vitatu na tayari wameshatembelea maeneo yanayofaa lakini mpaka sasa hakuna utekelezaji na pindi anapofuatiliahakuna jibu la moja kwa moja linalotolewa juu ya huduma ya maji.

Alisema pia tatizo jingine ni ucheleweshaji wa fedha za shughuli za maendeleo kutokufika kwa wakati na kuomba ngazi za juu kupitia kwa waziri husika kufika Usanda kujionea kero hiyo kwani hata mtandao wa maji ya ziwa victoria wamesahaulika na badala yake kata za jirani zimewekwa Samuye,Mwantini na Tinde.
KARENY. Powered by Blogger.