Habari za hivi Punde

WAKULIMA WALIA NA NDEGE WAITWAO KWELEA KWELEA KWA KULA MAZAO YAKIWA SHAMBANI




WAKULIMA  kata ya Usanda wilaya ya Shinyanga wameiomba  serikali kuchukuwa hatua za haraka  kuangamiza ndege waharibifu wa mazao kwelea kwelea ili kunusuru mazao yao kumalizwa na kuwepo tishio la kukumbwa na njaa pamoja na watoto kushindwa kuhudhuria masomo kwa kulinda ndege.

Wakiongea  na  waandishi wa habari waliotembelea kata hiyo,walisema mazao yao yanaliwa na ndege hao ukiwemo mpunga,mtama na uwele na kwamba wanahofia kukosa chakula kutokana na kushambulia kwa kasi na kubakiza mabua pekee.

Mkulima wa kijiji  cha Manyanda  Nyanda Jumanne  alisema hali kwa sasa ni mbaya na wanahitaji msaada wa haraka wa serikali, vinginevyo muda ukizidi kwenda kabla ya kuwadhibiti wakulima hawataambulia kitu na matokeo yake watakuwa wamepoteza nguvu zao bure.

Wakati mwingine inabidi watoto waende shambani kusaidie kufukuza ndege hao waharibifu na kushindwa kuhudhuria masomo,ambapo kwa sasa kwa kuwa shule zimefungwa kwa mapumziko ya sikuku ya pasaka watatumia muda huo kushinda shambani.

“ Makundi ya ndege wa haribifu wanatua kila kukicha tunawaona tunajitahidi kukaa mashambani kwa ajili ya kuwafukuza lakini wanatuzidi kwa kuwa ni wengi,bora serikali ingetuma ndege ya kunyunyizia dawa ili kuwauwa bila ya hivyo hakuna tunachokifanya”alisema Mussa.

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Abeid Aljabiri,alisema ni maafa makubwa kutokana na uharibifu unaofanywa na ndege hao na kuitaka serikali kusikia kilio cha wakulima ,kupeleka ndege ya kunyunyizia dawa haraka kwa kuwa muda unavyozidi kwenda ndivyo madhara yanatokea zaidi.

Alisema ndege hao kwelea kwelea wanaharibu mazao ya mpunga ,mtama na uwele wameharibu zaidi mazao katika kijiji cha Shagaluba,Manyada,Nzagaluba,Singita na Igaganulwa na hali ni mbaya katika vijiji hivyo ambapo wakati mwingine wazazi wamekuwa wakiwazuia watoto kwenda shule ili walinde ndege.

  

0 Response to "WAKULIMA WALIA NA NDEGE WAITWAO KWELEA KWELEA KWA KULA MAZAO YAKIWA SHAMBANI"

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.