WATOTO na akina mama manispaa ya Shinyanga wameandamana kwa lengo la kupinga ukatili dhidi ya watoto wa kike uliofanywa na kundi la waharamia wa kiislamu linalojulikana kama boko haramu lililopo nchini Nigeria mara baada ya kuwateka wanafunzi zaidi ya 270.
Maandamano hayo yalishirikisha pia shirika lisilo la kiserikali la AMSK FOUNDATION la mjini Shinyanga linalojihusisha na shughuli za kutetea ukatili dhidi ya watoto wa kike na akina mama huku mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Lilian Kowfie akieleza kuwa wameamua kufanya hivyo ili kukemea vitendo viovu vinavyofanywa kwa watoto wa kike.
Pia alisema kuwa shirika hilo limeguswa na kusikitishwa juu ya watoto wa kike waliotekwa huko nchini Nigeria jimbo la Borno mnamo tarehe 15 April mwaka huu ambapo zaidi ya watoto 270 wa shule walitekwa na kundi la Mgamo la kiislamu Boko Haramu na kupelekwa kusiko julikana kwa madai kuwa watoto wa kike hawastahili kusoma.
“Tumeamua kuandamana kwa kushirikiana na wakazi wa mjini shinyanga na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya kidini na serikali ili kukemea vitendo viovu vinavyofanywa kwa watoto wa kike na kuonekana hawana haki ya kupata elimu kama watoto wa kiume.”alisema Kowfie.
Kowfie alisema tabia ya unyanyasaji dhidi ya watoto wakike imedhidi kushika kasi mjini shinyanga na sehemu nyingine duniani wameona vyema kukemea vitendo hivyo wakishirikiana na wananchi, viongozi wa serikali na Dini kutoa elimu kwa wananchi wa mjini humo kuachana na matendo ya kikatili yakiwemo pia mauaji ya vikongwe.
“Maandamano haya kwajili ya amani ambayo tunakemea vitendo vya kikatili vinavyofanywa juu ya watoto wa kike hapa nchini na Afrika kwa ujumla ambapo pia tunashirikiana na wenzetu wa Nigeria kulaani matendo ya kikatili na kulitaka kundi la Boko Haramu kuwaachia watoto hao iliwaendelee na masomo yao” alisema Kowfie.
Naye mkuu wa wilaya ya Shinyanga AnnaRose Nyamubi aliwataka wakazi wa mjini humo kuacha kuendekeza mila potofu zilizopitwa na wakati kwa kuacha kuwasomesha watoto wa kike na kuwapeleka kwenye machungo huku wengine wakiozeshwa wakiwa na umri mdogo.
Nyamubi alisema tatizo la mkoa wa shinyanga ambalo lenye idadi kubwa la kabila la wasukuma wamekuwa wakiendekeza mila na desturi za mababu zao za kutowasomesha watoto wakike wakiamini watoto hao ni wakuolewa na hawawezi kuleta maendeleo, na kusema kuwa mila hizo zinafaa kupingwa vikali.
0 Response to "WATOTO NA AKINA MAMA WAANDAMANA KUPINGA UKATILI UNAOFANYWA NA KIKUNDI CHA BOKO HARAMU"
Post a Comment