WAFUGAJI wawili wa kabila la Kitaturu wa kijiji cha Rukale Kata ya
Bukundi wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu wameuawa kwa kupigwa risasi na
kisha kuporwa mifugo yao waliyokuwa wakichunga katika kijiji cha
Kakesio wilaya ya Ngorongoro mkoa wa Arusha na wafugaji wanaodaiwa wa
Kabila la Wamasai.
Tukio hilo limetokea Agosti 15 mwaka huu majira ya saa 4:00 asubuhi
wakati wafugaji hao wakiwa wanachunga mifugo yao ipatayo 40 katika
eneo hilo ambalo liko mpakani mwa mikoa hiyo na limekuwa na mgogoro
kwa muda mrefu.
Akizungumza jana na Waandishi wa habari mjini Mwanhuzi wilayani Meatu,Diwani
wa Kata ya Bukundi,Joseph Masibuka alisema kuwa waliouawa ni wafugaji
walioko katika eneo lake la utawala ambao ni wanaume na aliwataja kwa
majina ya mwanzo kuwa ni Ruida na Rewita ambao wote wanakadriwa kuwa
na umri wa miaka 35.
Alisema kuwa mara baada ya wafugaji hao kuuawa wenzao walipata taarifa
na kuanza kufuatilia mifugo hiyo ambayo ilikuwa eneo la wilaya ya
Ngorongoro na hapo mapigano yalipoanza kwa kutumia silaha za jadi na
inasemekana katika mapigano hayo mfugaji mmoja wa kabila la Wamasai
aliuawa.
Aliendelea kueleza kuwa taarifa hizo zilitumwa katika kituo cha polisi
cha wilaya ya Meatu na ndipo askari polisi walifika eneo la tukio
wakikutana na askari polisi wenzao kutoka wilaya ya Ngorongoro na
kutuliza mapigano hayo huku wakiendelea kutafuta mifugo hiyo
iliyoibiwa na walioshiriki mauaji hayo kwa kutumia risasi za moto.
Diwani huyo aliitaka serikali kuupatia ufumbuzi wa mgogoro huo wa
kugombea eneo la malisho kati ya wafugaji wa maeneo hayo kwani umekuwa
ni wa muda mrefu na bado haujapatiwa ufumbuzi.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Meatu,Dk Shali Shaku alikiri
kupokea miili ya wafugaji hao waliouawa na walichukua jukumu la
kuwazika baada ya ndugu zao kutofika kuuichukua miili hiyo.
‘Ni kweli tulipokea miili ya wafugaji hao wa kabila la Wataturu
iliyoletwa na askari polisi tumeihifadhi hapa katika chumba cha
kuhifadhia maiti kwa muda wa siku tatu na ndugu zao hawakuweza kufikia
kuzichukua kwa kuwa zilikuwa zimeharibika vibaya tumeaamua kuizika
jana”Alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu,Charles Mkumbo alisema kuwa kimamlaka
hawezi kulizungumzia suala hilo kwani limetokea ndani ya Mkoa wa
Arusha na hivyo kumwomba Mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha.
|
0 Response to "WAFUGAJI WAWILI KABILA LA KITATURU WAUWAWA NA KUPORWA NG'OMBE"
Post a Comment