Dar/Dodoma. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe leo atasindikizwa na
mawakili watano atakaporipoti Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dar es
Salaam alikoitwa kuhojiwa kuhusu kauli yake ya kuitisha maandamano nchi
nzima kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Mawakili hao wataongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Profesa Abdallah
Safari, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, Halima Mdee, Mabere
Marando na Peter Kibatala, huku makada wa chama hicho wakialikwa
kuandamana naye kumsindikiza.
Mbowe alitoa kauli hiyo katika Mkutano Mkuu wa chama hicho Septemba 14,
mwaka huu, akisema maandamano hayo yatafanyika katika siku ambayo
itapangwa katika mikoa yote.
Siku moja baadaye, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Kamishna
Paulo Chagonja alimkemea akisema iwapo atafanya hivyo, hatua za kisheria
zitachukuliwa. Pia, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI)
alimwandikia barua akimwita kuhojiwa.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema jana kwamba uamuzi huo
ni moja ya maazimio matatu ya kikao cha kwanza cha Kamati Kuu (CC) ya
chama hicho iliyokutana Dar es Salaam juzi.
“Mbowe ameitwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kesho (leo). Polisi
wameandika barua ya wito huo lakini hawajasema kosa lake ni nini.
Itakuwa saa tano asubuhi na atakwenda na mawakili wote wa chama,”
alisema Dk Slaa mbele ya viongozi wote wa sekretarieti mpya ya chama
hicho.
Akizungumzia wito huo jana, DCI Mngulu alisema ingawa leo atakuwa
Songea, ofisi yake ina watumishi wengi na kwamba ameshawasiliana naye
kwa ujumbe kumfahamisha hilo.
Katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika
alisema, “Tunawaomba wanachama wa Chadema kujitokeza Makao Makuu ya
Polisi ili kumsindikiza mwenyekiti atakayekuwa akihojiwa.”
Kwa upande wake, Lissu alisema katika barua ya wito, polisi wametaja
vifungu vya sheria, lakini hawakueleza kosa la Mbowe ni nini, jambo
ambalo linaonyesha jinsi wanavyofanya kazi nyuma ya kivuli cha chama
tawala, CCM.
Akizungumzia madai hayo, Mngulu alisema Kifungu cha 10 cha Sheria ya
Makosa ya Jinai kinajieleza wazi. Kifungu hicho kinazungumzia kudhamiria
kutenda kosa.
Maandamano
Akizungumzia maandamano hayo, Dk Slaa alisema tarehe rasmi itatajwa
baada ya viongozi wa Ukawa kukutana... “Maandamano yatafanyika nchi
nzima, tayari taratibu zimeanza kufanywa mikoani. Tutaeleza tarehe hiyo.
Tumepinga kwa maneno tukitaka Bunge lisitishwe lakini wenzetu wameweka
pamba masikioni. Sasa tunaonyesha chuki na hasira, polisi watambue kuwa
wao wapo 35,000 na wananchi wapo milioni 45.
“Tumenyimwa vibali katika mikutano yetu iliyopita sasa safari hii
wakikataa kutupa kibali tutaandamana tu. Azimio la Kamati Kuu haliwezi
kuvunjwa na Chagonja kwa sababu maandamano ni haki yetu na tumeshafanya
maandamano 100 ya amani nchini.”
Ukawa
Kuhusu ushirikiano wa vyama vinavyounda Ukawa, Dk Slaa alisema hilo ni
azimio la pili la Kamati Kuu ambayo imebariki ushirikiano huo kuanzia
katika Uchaguzi wa Serikali za Mtaa na Uchaguzi Mkuu 2015.
“Kamati Kuu imeunda kamati ndogo itakayoongozwa na Profesa Safari
ikiwajumuisha Benson Kigaira, Mnyika na John Mrema kuangalia namna
ushirikiano huo utakavyokuwa. Kamati hiyo imeanza kazi leo (jana),”
alisema.
Alisema azimio la tatu la Kamati Kuu ni kuhakikisha kuwa Ukawa wanaidai
Katiba ya wananchi na kwamba wanatembea nchi nzima kueleza uchakachuaji
wa Rasimu ya Katiba uliofanywa na CCM bungeni.
LHRC yawavaa polisi
Katika hatua nyingine, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
kimesema Jeshi la Polisi limekurupuka kuzuia wafuasi wa Chadema
kuandamana kupinga kuendelea kwa vikao vya Bunge wakati chama hicho
hakijatoa taarifa rasmi kwa jeshi hilo.
Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Uwajibikaji wa kituo hicho, Imelda Urio
alisema alichofanya Mbowe ni kutangaza kusudio la kufanya maandamano na
kwamba hatua nyingine za kutoa taarifa rasmi kwa jeshi hilo zingefuata
baadaye.
0 Response to "MBOWE LEO AUNGURUMA MJINI DODOMA CHINI YA ULINZI MKALI WA POLISI."
Post a Comment