VIONGOZI
Wakuu wa Vyama vya siasa vyenye Wabunge vinavyounda Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) wamekuwa katika mashauriano ya zaidi ya mwezi
mmoja tangu tarehe 2 Agosti mwaka huu huku wakishauriana juu ya mwenendo
wa mchakato wa Katiba Mpya na jinsi ya kuwa na uchaguzi ulio huru na wa
haki hapo mwakani.
Akiongea
kwa niaba ya viongozi wengine wa kituo hicho, Mhe. John Cheyo amesema
kuwa Katika mashauriano hayo yaliyochukua sura ya Kamati ya Makatibu
Wakuu, Kamati ya Wenyeviti wa Vyama vya CCM, CHADEMA, CUF na
NCCR-Mageuzi katika hatua tofauti. Mhe. Cheyo ameeleza kuwa kamati zote
zilitoa taarifa zao kwenye vikao vya Viongozi Wakuu wa Vyama (Summit) ya
TCD ambayo wajumbe wake ni Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na Makatibu
Wakuu wa Vyama wanachama.
Mhe.
Cheyo aliongeza kuwa katika kutafuta maridhiano, Wenyeviti na Makatibu
Wakuu wa Vyama walifanya mashauriano na Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete siku ya Agosti 31 na tena Nane Septemba 8, 2014 hapa Ikulu ndogo
mjini Dodoma.
“Pamoja
na kazi ya msingi inayofanywa na Bunge Maalum la Katiba, mchakato wa
Katiba unaoendelea sasa hauwezi kutupa Katiba itakayotumika katika
Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuwa muda hautoshi kukamilisha mchakato na
kufanya mabadiliko yatakayohitajika ya Sheria, Kanuni na Taasisi
mbalimbali zitakazohitajika”, alisema Mhe. Cheyo.
Mhe.
Cheyo aliendelea kwa kusema kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba mwisho wa mchakato ni kura ya maoni itakayofanyika mwezi Aprili
2015. “Kama itabidi kura irudiwe kwa mujibu wa Sheria iliyotajwa, kura
itarudiwa mwezi Juni au Julai 2015, muda ambao Bunge la Jamhuri ya
Muungano linatakiwa livunjwe kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba
2015 na ili Katiba Mpya itumike katika uchaguzi Mkuu utakaokuja, itabidi
uhai wa Bunge na Serikali uongezwe zaidi ya 2015, jambo ambalo
hatuliungi mkono”, alisisitiza Mhe. Cheyo.
Mhe.
Cheyo amesema kuwa Bunge Maalum la Katiba kwa sasa linafanya kazi kwa
mujibu wa Tangazo la Serikali (Government Notice) Na 254 lililotolewa na
Mhe. Rais Kikwete tarehe 1 Agosti, 2014. “Tangazo hilo litatumika hadi
tarehe 4 Oktoba, 2014 ambapo Katiba inayopendekezwa inategemewa
kupatikana, Wajumbe walikubaliana hatua hii iachwe ifikiwe”, alisema
Mhe. Cheyo.
Kuhusiana
na Kura ya maoni, Mhe. Cheyo ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba baada ya Bunge hilo kumaliza kutunga Katiba,
ingefuata hatua ya kura maoni kuthibitisha Katiba. “Kwa kutambua kuwa
hatua ya kura ya maoni italazimisha uchaguzi mkuu 2015 kuahirishwa, basi
hatua hii iahilishwe, na mchakato wa Katiba uendelee baada ya Uchaguzi
Mkuu wa 2015”, alisema Mhe. Cheyo.
Sambamba
na hayo, Mhe. Cheyo ameishauri Serikali kuchukua hatua za kisheria ili
matayarisho kwa ajili ya Uchaguzi wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa, yaanze
haraka iwezekanavyo ili uchaguzi ufanyike mapema hapo mwakani. Aidha,
amegusia kuhusu Mabadiliko ya 15 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya 1977 akasema kuwa, kwa vile Uchaguzi Mkuu wa 2015 utafanyika
kwa kutumia Katiba ya 1977, kuna umuhimu kufanya mabadiliko kidogo
(minimum reforms) katika Katiba pamoja na sheria ya Uchaguzi
yatayowezesha nchi kufanya uchaguzi huru na wa haki.
“Tayari mambo yafuatayo yamekubaliwa, kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi kusimam
ia
uchaguzi, Mshindi wa Uchaguzi wa Rais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50%
(50%+1)”, alisema Mhe. Cheyo. Viongozi hao Wakuu wa Vyama wamempongeza
Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa ujasiri wake na imani yake
katika kuimarisha demokrasia nchini na kuanzisha mchakato wa kuandika
Katiba Mpya ya nchi.
“Tunampongeza
kwa kukubali kukutana na kushauriana nasi kuhusu mambo ya muhimu kwa
mustakabali wa taifa letu kwa lengo la kudumisha amani, upendo na
mshikamano ili nchi yetu iende kwenye uchaguzi ikiwa ni nchi ya
kujivunia yenye amani, mshikamano na itakayokuwa na Uchaguzi Huru na wa
haki, lakini pia tunajipongeza sisi wenyewe Wakuu wa Vyama kwa kuwa
tumetoka mbali na misimamo yetu, lakini utaifa umetufanya tukubaliane
katika mambo ya msingi wa Taifa letu”, alipongeza Mhe. Cheyo
via>mwanaharakatimzalendo blog
|
0 Response to "VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA WAWEKA MASHAURIANO JUU YA CHAGUZI KUWA HURU NA HAKI."
Post a Comment