Wanafunzi wasioona wanaosoma katika shule ya msingi
Buhangija Jumuishi katika manispaa ya Shinyanga wanakabiliwa na upungufu wa
mashine za kujifunzia hali ambayo inaelezwa kuwapa wakati mgumu walimu
wanaowafundisha.
Hayo yamebainishwa jana na mkuu wa kitengo cha watoto
wenye ulemavu katika kituo hicho Bright Mduma ambapo alisema hivi sasa watoto
wasioona wapo 38, wavulana 25 na
wasichana 13,lakini mashine za kujifunzia zinazotumika ni 8 pekee kati ya 28
zilizopo.
Mduma alieleza kuwa kati ya mashine 25 za wasioona
nzima ni 8 pekee,20 ni mbovu na wamekuwa wakizitengeza mara kwa mara hivyo
kuwaomba wadau wa elimu na watoto kujitokeza kusaidia watoto hao.
“Tuna upungufu wa vifaa kwa watoto wasioona,mashine za
wasioona( Perking Brailler) nyingi zimeharibika,hata karatasi na kalamu maalum
kwa wasioona hazitoshi”,aliongeza Mduma.
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa kitengo alitaja
changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa meza na viti kwa wanafunzi na walimu
wanaofundisha watoto hao.
Kwa upande wake mwalimu
anayefundisha watoto hao Agnes Makambajeki aliiomba serikali na wadau
wengine kufika katika kituo hicho ili waone mazingira yasiyo rafiki kwa
wanafunzi hao ili waone umuhimu wa kuwasaidia.
Naye mwalimu mkuu msaidizi katika shule hiyo Pius
Lukala alisema walimu wanaofundisha watoto wasioona ni watatu pekee na
wanahitajika walimu wawili ili wawe watano wafundishe kuanzia darasa la kwanza
hadi la saba.
Shule ya msingi Buhangija Jumuishi iliyopo katika kituo cha kulelea
watoto wenye ulemavu wa ngozi,wasioona na wasiosikia hivi sasa ina watoto 275,
wasioona 38,wasiosikia 49 na wenye ulemavu wa ngozi 188.
Pamoja na shule hiyo kuwa na wanafunzi wenye ulemavu
pia wapo wanafunzi wasiokuwa na ulemavu 758.
Na Marunde Kadama.
0 Response to "WANAFUNZI WASIOONA (WENYE UPOFU) WATUMIA VIFAA VIBOVU KUJIFUNDISHIA KUANDIKA NA KUSOMA KITUO CHA BUHANGIJA SHINYANGA"
Post a Comment