Habari za hivi Punde

HII NI HATARI ASILIMIA 80 YA WAKAZI WA HALMASHAURI YA HANDENI MKOANI TANGA INAISHI BILA KUWA NA VYOO MAJUMBANI


                         Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemam
Asilimia 80 ya wagonjwa wanaolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni wanaugua homa ya matumbo kutokana na idadi kubwa ya wakazi wa wilaya hiyo kukosa vyoo na kujisaidia vichakani.

Hayo yalisemwa na mkuu wa wilaya hiyo, Muhingo Rweyemamu, wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mazingara, viongozi wa serikali ngazi ya wilaya na wa mashirika yasiyo ya kierikali kwenye ufungaji wa mradi wa World Vision Tanzania katika eneo hilo.



Alisema asilimi 80 ya wakazi wa wilaya ya Handeni hawana vyoo na badala yake wamekuwa wakijisaidia vichakani, hali ambayo inasababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira na magonjwa ya milipuko kwani uchafu huo umekuwa ukiingia kwenye vyanzo vya maji yanayotumiwa na binadamu.

Alisema kutokana na tatizo la ukosefu wa maji linaloikabili wilaya ya Handeni, wapo baadhi ya watu wanachota maji katika mabwawa na kisha kunywa bila ya kuchemsha hali ambayo imekuwa ikisababisha kupatwa na magonjwa ya matumbo kwani maji hayo si salama kutokana na mvua kusomba sehemu kubwa ya vinyesi kutoka katika milima na kupelekwa katika mabwawa hayo.

“Kusema kweli hili ni tatizo na ni tatizo kubwa...elimu inahitajika kutolewa, lakini maafisa afya nao wafanye kazi yao kwa kutumia sheria ndogondogo za halmashauri kuwachukulia hatua wote wasio na vyoo ...kikianza kipindupindu hapa ni maafa”  alisema Mkuu huyo wa wilaya.

Awali akielezea kero ya maji ilivyopunguzwa katika maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji, Meneja wa World Vision Tanzania, Kanda ya Mashariki,  Sylivester Masanja, alisema katika eneo la Mazingara wamefanikiwa kuongeza huduma hiyo kutoka asilimia 28.5 hadi kufikia asilimia 38.5, huku baadhi ya shule na zahanati pamoja na wakazi wa baadhi ya vijiji wanavuna maji kwa njia ya mabwawa na matanki .

Masanja alisema hatua hiyo imeweza kupunguza tatizo hilo kutoka asilimia 36 hadi 62 kwa wakazi wa eneo hilo .

0 Response to "HII NI HATARI ASILIMIA 80 YA WAKAZI WA HALMASHAURI YA HANDENI MKOANI TANGA INAISHI BILA KUWA NA VYOO MAJUMBANI"

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.