Hatimaye mwili wa Rosemary Marandu uliohifadhiwa katika chumba
cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa siku 53 umezikwa
huku maziko hayo yakigubikwa na utata na kuhudhuriwa na wanaume sita.
Mazishi hayo yalifanyika juzi saa 10:30 jioni
katika Makaburi ya Karanga mjini hapa na hakuna aliyehudhuria kati ya
baba wala mama wa marehemu.
Taarifa za kufanyika kwa siri kwa maziko hayo
zililifikia gazeti hili saa 10:40 jioni na waandishi walipofika
makaburini, waliambulia kukuta mishumaa iliyokuwa ikiwaka ikiwa imewekwa
juu ya kaburi na hakukuwa na mtu hata mmoja.
Mashuhuda wa tukio hilo, waliozungumza na gazeti
hili, walidai kuwa waliyaona magari mawili yakiingia makaburini hapo,
moja likiwa limebeba maiti na kushuhudia watu sita wakishuka katika
magari hayo ambao waliuzika mwili huo.
Hata hivyo, bado kuna utata kuhusu nani hasa
aliyefanya maziko hayo baada ya baba wa marehemu kudai ni mtoto wa
marehemu aitwaye Witness Marandu na mkewe Felicia akikanusha.
Maziko hayo yamefanyika ‘chapchap’ wakati marafiki
wa karibu na Marandu walipokuwa katika jitihada za mwisho za
kumshawishi aukabidhi kwa mama wa marehemu juzi mchana ili auzike.
Kauli ya Baba wa Marehemu
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu juzi
usiku kutoka wilayani Rombo, baba wa Rosemary, Flavian Marandu alisema
mtoto wa marehemu aliyemtaja kwa jina la Witness Marandu (17), ndiye
aliyeuchukua mwili huo na kwenda kuuzika.
Marandu alisema mtoto huyo alimfuata akiwa
amefuatana na ndugu wengine ambao hakuwataja akiomba apewe mwili wa mama
yake ili akauzike.
Alidai kuwa awali aliwapa uhuru wa kuchagua sehemu
ya kwenda kuzika katika moja ya mashamba yake yaliyoko Kitirima
Kingachi wilayani Rombo au katika makaburi ya umma watakayoona yanafaa.
Marandu alisema baadaye akiwa amepumzika akiugulia
maumivu ya kutoa jino, wanaukoo hao pamoja na mtoto wa marehemu
walimpigia simu na kumshukuru kwamba wameshazika salama.
Mgogoro huo wa kugombea maiti ni wa pili kuhusisha ukoo wa akina
Marandu, miaka takriban 10 iliyopita, maiti nyingine ya mwanaukoo huo
ilikaa mochwari kwa zaidi ya siku 90 baada ya kutokea mgogoro unaofanana
na huo.
Mama ageuka mbogo
Hata hivyo Felicia Nkya ambaye ni mama mzazi wa
marehemu aliliambia gazeti hili si kweli kuwa mjukuu wake (Witness)
ndiye aliyeuchukua mwili huo na kwenda kuuzika.
Alisema madai ya mumewe kuwa mjukuu huyo alimfuata
juzi kuomba akauzike mwili huo hayana ukweli kwani mpaka siku hiyo,
Witness alikuwa yuko shuleni mkoani Mbeya.
0 Response to "MWILI WA BINADAMU ULIOKAA MOCHWARI KWA ZAIDI YA SIKU 50 HATIMAYE UMEZIKWA KIMYAKIMYA -MKOA WA KILIMANJARO MOSHI"
Post a Comment