Habari za hivi Punde

UKATILI KWA WATOTO MKOANI SHINYANGA BADO CHANGAMOTO KUBWA INAKADIRIWA KWA SIKU WATOTO 16 MKOANI SHINYANGA HUPEWA UJAUZITO.


Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinaendelea  kushika kasi mkoani Shinyanga huku takwimu zikionesha kuwa watoto 16 wanapewa ujauzito kila siku na wengine 500 wakiachishwa shule kila mwaka kutokana na mimba na ndoa za utotoni.

Takwimu hizo zimetolewa wiki hii na Mkurugenzi wa Shirika la lisilo la kiserikali linaloteteaa haki za watoto na wanawake la AGAPE mkoani Shinyanga John Myola (PICHANI)wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga.

Alisema  kwa mujibu wa  utafiti uliofanywa na shirika la  UNICEF mwaka 2012 mkoa wa Shinyanga katika wilaya ya Kishapu,Shinyanga vijijini na Kahama pekee watoto 16 wanapewa ujauzito huku watoto 500 wakiachishwa masomo kwa sababu ya mimba na ndoa za utotoni.

Alisema pamoja na takwimu kuonesha kukithiri kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto lakini kesi za mimba na ndoa za utotoni  zinakwamishwa na vyombo vya uamuzi vinavyoendekeza rushwa kukwepesha kesi hizo.

“Watu wa kwanza kupiga vita ukatili wa watoto walipaswa kuwa watu wa mahakama,mtuhumiwa akipelekwa katika vyombo vya maamuzi,unakuta mzaha mzaha,unakuta mazingira ya rushwa,nenda katika mahakama zetu zote wanakula rushwa kuangamiza haki ya mtoto”,alisema Myola.

Hata hivyo alisema ni vyema sasa kukawepo mahakama za watoto ili mambo ya watoto yakazungumzwe pale kwani haki za watoto zinaangamizwa kwa kukosa mahali pa kusikilizwa huku makarani na mahakimu wakiendekeza rushwa.

“Niwaombe  waandishi wa habari ongezeni sauti ya pamoja ,inapotokea kesi ya mtoto fuatilieni hadi mwisho,najua hata wale waheshimiwa mahakimu wanaokula rushwa wanapoona waandishi wanafuatilia kesi ya mtoto,nina imani wanaweza kushtuka na hii tabia mbaya”,aliongeza Myola.

Hali kadhalika alisema pamoja na vyombo vya maamuzi kuchangia kuongezeka kwa ukatili dhidi ya watoto aliwataka wanajamii kushiriki kwa pamoja kupiga vita vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa watoto kwani taifa linaharibika kwa kuendekeza mzaha.

Na Kadama Malunde-Shinyanga
KARENY. Powered by Blogger.