Na Kareny Masasy
Shinyanga.
CHAMA cha wafanyakazi
wa migodi, nishati, ujenzi na kazi nyinginezo (TAMICO) kinatarajia kuwafikisha
mahakamani viongozi waandamizi wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu unaomilikiwa
na African Barrick Gold mine,(ABG) kwa tuhuma za kuwashawishi watumishi wa
mgodi huo kusitisha uanachama wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake, mjini
Shinyanga, katibu wa TAMICO, kanda ya magharibi, Benjamini Dotto alisema
walifikia uamuzi huo kufuatia uongozi wa Mgodi kusambaza fomu maalumu kwa
watumishi hao ikielekeza kuwashawishi kujiondoa uanachama TAMICO.
Aliwataja viongozi hao kuwa ni pamoja na meneja mkuu wa
mgodi huo, Peter Burger, meneja kitengo cha mahusiano kazini rasilimali watu,
Onesmo Kabeho, meneja kitengo cha rasilimali watu, Antony Mosha na meneja
ustawi wa kampuni hiyo, Gath Boersma.
Alisema kwa pamoja viongozi hao wametumia nafasi zao za
uongozi kuwashawishi wafanyakazi wapatao 651, kusitisha uanachama wao TAMICO
kwa maslahi yao binafsi ikiwemo kuaandaa namna ya kuwafukuza kazi na kuwanyima
haki zao.
“Tumeamua kuwafikisha mahamani kutokana na na viongozi hao
kuwashawishi wafanyakazi kusitisha uanachama TAMICO ambapo januari 10, mwaka
huu Bw. Mosha aliwasainisha barua hizo watumishi 375 kwa barua yenye kumbukumbu
namba, BGML/HR/2014” alisema katibu huyo.
Aidha, alimtaja mwingine kuwa ni meneja ustawi wa kampuni
hiyo, Gath Boesma, ambaye aliwasainisha watumishi 214, novemba 9, mwaka jana,
kwa barua yenye kumbukumbu namba BGML/HR/2013 na watumishi 62 kwa barua yenye
kumbukumbu namba BGML/HR/2013 ya novemba 8 mwaka jana
Katika hatua nyingine, katibu huyo alisema (TAMICO)
imefungua kesi mbili dhidi ya kampuni hiyo ya madini katika tume ya usuluhisi
na uamuzi(CMA) mjini Shinyanga.
Alizitaja kesi hizo kuwa ni pamoja na kesi ya kwanza
yenye kumbukumbu namba CMA/SHY/3/2014 kikiwa chama hicho kinaiomba tume
ibatilishe notisi ya mwajiri aliyoitoa kwa chama ikiwa na kusudio la kuvunja
mkataba wa utambuzi ambapo katika kesi ya pili yenye kumbukumbu namba
CMA/SHY/4/2014 chama kinaomba kukamilishwa na kufungwa kwa mkataba wa hali bora
iliyotakiwa kufanya hivyo tangu mwaka 1999.
Katibu huyo wa TAMICO kanda ya magharibi alisema chama hicho
kilifikia maamuzi hayo baada ya kugundua kwamba uongozi wa kampuni hiyo ya
Bulyanhulu haukufuata taratibu za kisheria, katika kufikia hatua ya kutoa
notisi ya kuvunja mkataba wa utambuzi ambapo pia mwajiri amechelewesha
kumalizika kwa majadiliano ya mkataba wa hali bora hivyo kuwanyima nafasi
wafanyakazi ya kuongezeka kwa maslahi yao.
Aidha, Bw. Dotto alifafanua kuwa mwajiri huyo ameonesha nia
mbaya katika kuvunja mkataba huo kwa kutengeneza fomu hizo haramu ambazo kwa
kushirikiana na kikundi alichokiita haramu cha NUMET wamekuwa wakiwaondolea
wafanyakazi nguvu ya kujadiliana.
0 Response to " TAMICO YATARAJIA KUWABURUZA MAHAKAMANI VIONGOZI WAANDAMIZI BULYANHULU."
Post a Comment