Habari za hivi Punde

WAKAZI WA KIJIJI CHA NGAGANULWA KATA YA USANDA WAKABILIWA NA UHABA WA MAJI.

Na  Kareny  Masasy
Shinyanga.
WAKAZI  wa kijiji cha Ngaganulwa  kata  ya Usanda wilayani Shinyanga wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa upataji maji safi na salama ya kunywa ambapo wamekuwa wakitumia maji  yaliyojitenga  kwenye mito hali ambayo imeweka kuhatarisha maisha yao kwa kupatwa na mlipuko wa magonjwa kama kuhara na kipindupindu.
Wakiongea na mwandishi wa habari  aliyetembelea kwenye kata hiyo  baadhi ya wananchi  walisema kuwa kilio cha muda mrefu kwa uhaba wa maji kipo ambapo huwalazimu kunywa maji yasiyo salama huku wangine wenye uwezo hununua dumu moja la lita ishirini  shilingi 500.
Wakazi hao walisema kuwa imekuwa ni ndoto kwao kupata maji safi na salama ya kunywa kwa muda wa miaka mingi huku wakiiomba serikali  kuwafanyia ufumbuzi wa kuwachimbia  visima virefu ili waweze kuondokana na changamoto hiyo ikiwa awali waliweza kuchimbiwa visima vifupi ambavyo  havihifadhi maji iwe masika au kiangazi.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho  Mhoja Daudi alisema kuwa   maji salama yanayasikia mjini na sio ndani ya kijiji hicho  hivyo wanaiomba serikali  kuwawezesha  kwa visima virefu au kuwachimbia mabwawa yakuweza kuhimili hata kilimo cha umwagiliaji  kwa  kuweze kupata maji safi na salama na kupunguza tatizo la njaa.
 Naye diwani wa kata hiyo  Ndaji  Al-Jabri  alisema kuwa changamoto ya uhaba wa maji sio tu kwa kijiji hicho bali ni kata yote  ambayo haina mabomba,visima virefu wala mabwawa  bali kulikuwepo na visima vifupi ambavyo hukauka mapema hata kipindi cha masika pia  kunakuwa hakuna maji wananchi kulazimika kutumia maji ya mitoni ambayo sio salama kwa kutembea umbali mrefu kuyapata.
Alisema  tangu mwaka 2007  tatizo hilo lilielezwa na kupangiwa bajeti,kuwekewa michoro  kwaajili ya ujenzi wa mabwawa   kwenye vijiji viwili vya Ngaganulwa na Singita  lakini utekelezaji wake umekuwa ni mugumu  mpaka leo hii michoro hiyo ipo.
“Changamoto ya ukosefu wa maji katika kata yangu ipo, ninacho hitaji hapa ni  visima virefu  ambavyo wananchi wataweza kupata maji safi na salama ya kunywa ,mabwawa ili kuweza kumudu kilimo cha  umwagiliaji  kama hayo yote hatata tekelezwa itabaki kuwa ni tatizo njaa haitakoma kwa wananchi pia maisha yao kuwa hatarini kwa kukosa maji safi na salama ya kunywa”alisema Diwani huyo.
KARENY. Powered by Blogger.