BAADHI ya watumishi
katika halmashauri ya manispaa ya Shinyanga wameanza kuihujumu manispaa hiyo
kwa kutumia mbinu ya kufungua kesi dhidi ya manispaa hiyo na kuiba nyaraka za ofisi
ili kujipatia kipato.
Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani naibu mstahiki meya David Nkulila alisema hivi sasa halmashauri hiyo
inaandamwa na kesi nyingi za ajabu zenye
lengo la kuihujumu manispaa kwa kushindwa kuiba mapato matokeo yake kutumia
mbinu hizo.
Alisema manispaa inataka kuchezewa na watu kwa kuanza kuihujumu
kwa kuanzisha makosa yasiyoeleka na kwamba kwa mujibu wa taarifa
zinazohisiwa,zinazotia mashaka hujuma hizo zinafanywa na watumishi wa
halmashauri hiyo.
“Data zinazohisiwa,zinazosemekana,zinazotia
mashaka,watumishi wanahusika,Kesi nyingi sasa zinataka kuiandama
halmashauri,mdau yupo anaambiwa anzisha kesi na kesi inaenda kushindikana,mtu
huyo anadai alipwe na halmashauri, na hayo madai yanavyosemekana ni mgao wa
watu,hizo ni hujuma kwa pesa za wananchi”,alieleza Nkulila.
Akifafanua zaidi alisema menejimenti ya manispaa hiyo
imekosa nidhamu ya siri kwani wamekuwa wakitoa nyaraka za siri na kwamba sasa
wamebuni njia nyingine ya ulaji kwa kuanzisha kesi badala ya kuwajibika.
Pia aliwataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa
nidhamu,kuridhika na walichonacho,kuwatumikia wananchi na kuwajibika kila mtu
kwa nafasi yake kama inavyopaswa kwa kufuata yaliyoelekezwa.
Naye katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga Boniface Chambi
aliwataka watumishi wa umma kutunza siri za ofisi na endapo mtu anaona kazi ya
serikali ni ngumu aondoke taratibu badala ya kuchezea nyaraka za serikali.
0 Response to "BAADHI YA WATUMISHI MANISPAA WADAIWA KUIHUJUMU KWA KUIBA NYARAKA ZA SIRI"
Post a Comment