Habari za hivi Punde

MAUAJI YA ALBINO YAMEPUNGUA ,YANAYOENDELEA NI MAUAJI YA KUWANIA URITHI,ARDHI PAMOJA NA IMANI ZA KISHIRIKINA



SERIKALI mkoani Shinyanga  imeeleza kupungua kwa mauaji ya albino kwa kiwango kikubwa  ikiwa kwa mwaka jana hakuna tukio lolote lililotokea la mauaji hayo isipokuwa mauaji ya watu wengine wakimweo vikongwe kuendelea kujitokeza  kwa kusababishwa  kugombea  mirathi,ardhi pamoja na  imani za kishirikina.

Hayo yalisemwa  na mkuu wa mkoa wa Shinyanga  Ally Rufunga wakati akiongea na waandishi wahabari katika ukumbi  wa mkoa huku akieleza  kuwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) yamepungua kwa asilimia 100 huku mauaji vikongwe na watu wengine yamepungua kwa asilimia 96.

Alisema hali ya ulinzi na usalama  kwa sasa ni shwari ikiwa mwaka wa 2012 kulitokea tukio moja la mauaji wilayani Kahama ,ambapo mwaka wa 2013 hakuna tukio lolote lililotokea  ila hali ya mauaji ya vikongwe na watu wengine imeendelea kujitokeza kwa sababu ya w engine kuwania mali,mirathi na imani za kishirikina.


“Kweli maeneo  hasa ya  pembezoni matukio ya mauaji bado yanajitokeza hivyo mikakati iliyopo kila halmashauri kutenga fedha kwaajili  ya kuajiri mgambo ,kujenga vituo vidogo vya polisi na  elimu itolewe kwa wananchi ili kuondokana na changamoto hizo.”alisema Rufunga.

Hata hivyo alisema kuwa katika wilaya zote za mkoani hapa wilaya ya Kahama ndio inaongoza kwa matukio ya mauaji  ya aina zote ambapo hata kuuliwa  ama kujeruhiwa kwa vikongwe na albino  kumetokea zaidi kwenye wilaya hiyo  na  watu waliohusika kwa vitendo vya mauaji ya albino walitokea huko na kuhukumiwa kunyongwa. 

Hata hivyo jeshi la polisi katika taarifa zake  lilieleza  kuwa  mkoa huu umekuwa  wa pili katika rekodi yake  kwa mauaji  mbalimbali yanayotokana  na  imani za kishirikina  na kuwania mali za urithi  hasa kwa kuwauwa wanawake  wenye umri wa kati ambao sio vikongwe.

Jeshi hilo pia lilisema kuwa Kwa sasa mauaji hayo hayachagui kama zamani bali wanauwawa wanawake  ndani ya familia zao  ikiwa  hapo awali  dhana iliyokuwepo ni mauaji ya vikongwe pekee hivyo jamii inatakiwa  kuwa  wawazi kwa kuwafichua wanaofanya vitendo  hivyo kwani hata wakiwa wanawafahamu imekuwa   vigumu kuwafichua hiyo ndio changamoto kubwa.

 Ikiwa  wiki iliyopita  watu  wawili waliuwawa kikatili kwa kucharangwa mapanga na watu wasiojulikana kwa kuwavamia nyumbani kwao  majira ya  usiku  huko  katika kijiji cha Ngokolo wilayani Kahama mkoani Shinyanga huku chanzo cha mauaji hayo kutofahamika.

Kwa mujibu  wa taarifa ya kamanda wa jeshi la polisi  mkoani hapa Evarist Mangalla  alisema kuwa  watu  hao ni mama na mwanaye  waliofahamika kwa majina  ya Helena Charles(30)   na Mlu Nambo ( 50) walivamiwa usiku na watu wasiojulikana huku wakiwa mkononi wameshika mapanga na kuanza kuwacharanga  wakati wakijiandaa na  chakula cha usiku huo.
 

0 Response to "MAUAJI YA ALBINO YAMEPUNGUA ,YANAYOENDELEA NI MAUAJI YA KUWANIA URITHI,ARDHI PAMOJA NA IMANI ZA KISHIRIKINA"

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.