Habari za hivi Punde

ZAIDI YA ASILIMIA 80 YA VIJANA NCHINI HUFANYIWA UKATILI

ZAIDI ya asilimia 80 ya vijana nchini  wenye umri  kati ya miaka   13 hadi 24 wameripotiwa kunyanyaswa kingono,kudhalilishwa kihisia na kujeruhiwa walipokuwa watoto chini ya umri wa miaka 18 huku matukio hayo  yakishamiri zaidi sehemu za shule na kuathiri uwezo wa
 watoto kielimu.
 
 Hayo yalielezwa jana na meneja wa shirika la  Save The Children mkoa wa Shinyanga Augustino Mwashiga wakati wa uzinduzi  mradi wa kudhibiti ukatili dhidi ya watoto,alisema utafiti uliofanywa na UNCEF mwaka 2008  ulibaini kuwepo ukatili huo hapa nchini huku wastani wa matukio nane hadi 10 ya ukatili hutokea kila mwezi mkoani
 humo.
 
 Mwashiga alisema asilimia 30 ya wasichana na wavulana asilimia 14 waliwahi  kunyanyaswa kingono chini ya umri wa miaka 18 ikiwa ni pamoja na kuchomwa moto mikono na kupigwa,ambapo ameitaka jamii kutoa ushirikiano kuwafichuwa wanaofanya ukatili  huo.
 
 “Takwimu zinaonyesha tatizo la unyanyasaji wa watoto nchini Tanzania ni kubwa na watoto wengi wamefanyiwa ukatili kwa kunyanyaswa kingono,kihisia na kisaikolojia,matukio ambayo katika utafiti wetu ndiyo tunayabaini”alisema
 meneja Mwashiga.
 
 Akizungumza kwenye mkutano huo afisa ustawi wa jamii mkoa wa Shinyanga Jesca Kagunila alisema alisema katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2013 ziliripotiwa kesi 100 za ukatili
kwa watoto wakiwemo wavulana 23 na wasichana 77 huku ubakaji ukiongoza kwa kuwa na kesi 34.
 
 Alisema ufinyu wa bajeti kwenye halmashauri ni moja ya kikwazo cha kushindwa kufuatilia matukio mbalimbali hasa maeneo ya vijijini na kuzitaka kuhakikisha wanatenga fungu kila mwaka ili elimu zaidi itolewe kwa jamii iweze
 kuondokana na vitendo hivyo vya ukatili.
 
  Akifungua mkutano huo katibu tawala mkoa wa Shinyanga Anselm Tarimo alilaani vikali tabia inayofanywa na baadhi ya wazazi kuwachungisha mifugo watoto  muda wa masomo kuwa ni ukatili kwa kuwa wanakosa haki yao ya msingi ya kupata
elimu ikiwa ni pamoja na kuwanyima chakula.
 
 Nao baadhi ya wanaharakati wa kutetea haki za watoto kutoka shirika la Pacesh John Shija na Perepetua Magoke walisemaumasikini ni moja ya chanzo cha kuwepo ukatili kwa kupatiwa
 fedha na kuficha matukio ya udhalilishaji.
KARENY. Powered by Blogger.