KUNDI kubwa la Tembo zaidi ya 40 kutoka
katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wamevamia katika makazi ya watu na
kufanya uharibifu mkubwa wa mazao pamoja na vyakula vilivyokuwa vimehifadhiwa
katika kijiji cha Mwachumu kata ya Girya Wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Diwani wa kata ya Girya Safari Lewa alisema kuwa tukio
hilo limetokea juzi majira ya saa 10:00 jioni katika kijiji hicho ambapo tembo hao
waliingia kwenye makazi ya watu na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao mbalimbali
yakiwemo Mahindi pamojana na Pamba katika mashamba ya wananchi.
Lewa alisema kuwa zaidi ya hekari 60 za mazao ya
Mahindi na Pamba zimeharibiwa vibaya na tembo hao na kwamba kwa sasa wananchi
wa kijiji hicho wanaishi kwa wasiwasi mkubwa wakihofia kushambuliwa na tembo
hao.
Alibainisha kuwa kutokana na wananchi hao kushambuliwa kwa
mazao yao na tembo pia watakabiliwa na upungufu wa chakula na ameuomba
uongozi wa hifadhi hiyo kuwasaidia wananchi waliodhulika na tembo hao kuwaletea
chakula pamoja na kuja kuwatoa tembo hao katika maeneo ya makazi ya watu.
‘’Tuwe na usawa kwa wote pale wananchi waingizapo
ng’ombe katika eneo la hifadhi hutozwa faini kali pia na wao wanapaswa kutoa
fidia kwa wananchi wetu ambao wanaharibiwa mazao na wanyama’’alisema Lewa.
Mmoja wa wananchi hao kutoka kijiji hicho Mhoja Jilinge
alisema kuwa tembo hao walivamia jioni mashamba yao ikiwa mazao bado
hawajavuna na kuanza kushambulia hali ambayo inaonyesha kuwa
hifadhi hiyo imekosa uangalizi mzuri pia hofu iliyopo kumaliza mazao na
kudhuru watu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya
Bariadi Abdallah alikiri wanyama hao kuvamia maeneo hayo ambapo aliwaomba
wananchi na viongozi wa maeneo hayo ambako tembo wamevamia wawe wanatoa taarifa
mapema ili hatua za kuwarudisha hifadhini ziweze kuchukuliwa haraka.
0 Response to "KUNDI LA TEMBO LAVAMIA MAKAZI YA WATU NA KULA MAZAO YALIYOKUWA MASHAMBANI NA VYAKULA WALIVYOHIFADHI"
Post a Comment