ZAHANATI ya kijiji cha Singita kata ya Usanda wilaya ya Shinyanga inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji hali ambayo inayowalazimu mama wanaokwenda kujifungua kununua maji dumu la lita ishirini shilingi mia mbili ikiwemo ukosefu wa maabara.
Wakiongea na waandishi wa habari waliotembelea zahanati iliyopo kijijini hapo,walisema kuwa wanapokwenda kujifungua hulazimika kununua maji kwaajili ya kufulia nguo na kuoga jambo ambalo limekuwa ni changamoto kwao yakuwafanya kutumia gharama kubwa huku kipato chao ni kidogo.
Walisema kuwa Zahanati hiyo haina huduma ya maji hulazimika kununua dumu moja la lita ishirini shilingi miambili ambayo ndiyo changamoto kubwa ikiwemo ukosefu wa dawa mara kwa mara,maabara na baadhiya ya vifaa tiba ikiwa hulazimika kufuata vipimo vingine katika hospitali ya serikali ya mkoa au binafsi zilizoko mjini.
“Katika suala la maji tunatumia gharama kununua dumu moja shilingi 200 kwa kipindi hiki cha masika lakini msimu wa kiangazi maji huwa adimu tunalazimika kununua dumu moja mpaka shilingi 600 ili kuweza kuoga na kufua pindi tunapojifungua,isitoshe kuna uhaba wa dawa, maabara ya kupata vipimo vya magonjwa mengine kama kifua kikuu,kichocho na mengineyo”alisema mkazi wa kijiji hicho Hawa John.
Naye diwani wa kata hiyo Abeid Aljabir alikiri kuwepo kwa uhaba wa maji katika Zahanati hiyo ikiwa tayari kuna mambomba ambayo tangu yawekwe hayajawahi kutoa maji hivyo imekuwa ni changamoto kubwa katika jamii kununua maji huku kipato chao ni kidogo aliiomba serikali kuwapatia maji kutoka mradi wa ziwa Victoria ili kuondoa kero hiyo.
Kwa upande wake muuguzi wa zahanati hiyo Leticia Anthony alisema kuwa kweli Zahanati inachangamoto ya uhaba wa maji hivyo hata wao hulazimika kununua kwaajili ya matumizi ya usafi,pia akina mama hao wanapokuja kujifungua hulazimika kununua maji ya kuoga na kufulia dumu lenye lita ishirini shilingi 200.
“Kweli zahanati hii haina maabara,vifaa tiba,vifaa vilivyopo ni kwaajili ya upimaji malaria na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) ikiwa wastani wagonjwa kwa siku ni 60 hadi 70 zaidi ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano huja kwa maradhi ya malaria na wakubwa kwa maradhi ya kikohozi ambapo wanaokwenda kujifungua kwa mwezi hufikia zaidi ya 40”alisema Antony.
Naye ofisa afya kata ya Usanda Mussa Chande alisema kuwa Zahanati hiyo inahudumia vijiji vitano vya Singita, Shagaluba,Manyada, Nzagaluba, na Igaganulwa. ikiwa kwa kata nzima kuna idadi ya watu zaidi ya 15,000
0 Response to "ZAHANATI YA KIJIJI CHA SINGITA KATA YA USANDA YAKABILIWA NA UHABA WA MAJI,MAABARA NA DAWA."
Post a Comment