Habari za hivi Punde

ZAIDI YA ABIRIA 60 WANUSURIKA KUFA NA BASI LA NAJIMUNISA.



ZAIDI ya abiria  60 wamenusurika kufa huku majeruhi  wakiwa 52 baada ya basi la Supernajimunisa lenye namba za usajili T.242 BRJ walilokuwa wanasafiria kutoka Jijini Mwanza kuelekea jijini Dar es salaam kupinduka katika kijiji cha Busanda kata  ya  Usanda  mkoani  Shinyanga.

Ajali hiyo imetokea leo majira ya saa tatu asubuhi ambapo basi hilo aina ya scania mali ya kampuni ya Supernajimunisa  likitokea Mwanza kuelekea Dar es salaam likiwa na idadi ya abiria hao ambapo lilipasuka tairi la mbele kulia na kupinduka. ikiwa majeruhi katika ajali hiyo walikimbizwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu kwani wengine hali zao zilikuwa mbaya.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe alisema  hospitali ya mkoa wa Shinyanga imepokea majeruhi 52 ambapo kati yao majeruhi waliolazwa ni 22,ambao wanne kati yao hali zao ni mbaya ambao ni wanaume  wawili na wanawake wawili.

Dkt Kapologwe alisema  kuwa kati ya majeruhi  hao waliopokelewa katika hospitali hiyo tayari majeruhi 30 wamesharuhusiwa kutoka hospitalini hapo.
Hata hivyo  baadhi ya majeruhi waliolazwa katika hospitali hiyo walisema ajali hiyo ilitokea baada ya tairi la mbele la basi hilo kupasuka na kusababisha basi kuingia mtaroni na kujeruhi abiria waliokuwa ndani ya basi.

“Mwendo  wa basi ulikuwa wa kawaida,tairi lilichomoka gari likapinduka ,kama lingekuwa katika mwendo kasi naamini lazima watu wangekufa,lakini hakuna aliyekufa katika ajali hii”,alisema Daudi Mapunda aliyekuwa anasafiri kutoka Mwanza kwenda Dar es salaam.

Kwa upande wake  Edina Shija ambaye ameumia kidevuni alisema basi lilikuwa katika mwendo wa kawaida huku akiwataka wahusika wa magari kujenga tabia ya kukagua vizuri vyombo vya usafiri ili kuepuka ajali zisizokuwa za lazima.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema  kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kwamba pamoja na kupasuka kwa tairi basi hilo lilikuwa katika mwendo kasi  huku uchunguzi ukiendelea.

0 Response to "ZAIDI YA ABIRIA 60 WANUSURIKA KUFA NA BASI LA NAJIMUNISA."

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.