MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA KISHAPU JUSTINE SHEKA.
HALMASHAURI ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imefanikiwa kurudisha kiasi cha shilingi billioni 2.1 zilizosemekana kuibiwa na baadhi ya watumishi wa idara mbalimbali wakishirikiana na watumishi wa benki ya NMB Manonga tawi la Shinyanga mjini,huku watumishi nane waliosimamishwa wakirejeshwa kazini.
Wakiongea kwenye baraza la madiwani lililofanyika jana katika ukumbi wa halmashauri hiyo ambapo kaimu mkurugenzi Amosy Zephania alieleza kwenye kikao hicho kuwa uongozi wa benki hiyo umekubali kurudisha kiasi hicho cha pesa ambacho kiliibiwa tangu mwaka 2007 hadi 2010 pindi mkaguzi wa hesabu za serikali (CAG) alivyobaini.
Zephania alisema kuwa katika upigaji mahesabu ilibainika kiasi cha shilingi billioni 2.1 kupotea kwa kuchukuliwa kutoka kwenye benki ya NMB ambapo uongozi huo umekubali kurudisha kiasi cha pesa hizo katika halmashauri baada ya kamati iliyoundwa kufuatilia suala hilo.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo kamati iliyokaa ya madiwani na uongozi wa halmashauri kwa mujibu wa taratibu na sheria umefanikiwa kuwarudisha watumishi nane kazini ambao walikuwa wamesimamishwa waliopisha uchunguzi kufanyika kutokana na kudhaniwa kuhusika na tuhuma ya wizi huo .
Hata hivyo mwenyekiti wa halmashauri hiyo Justine Sheka alisema kuwa fedha hizo ziliibiwa na kuifanya halmashauri kupata hati chafu mwaka 2012 kwa ubadhilifu uliofanyika hivyo kwa jitihada zilizofanyika kwa kushirikiana na naibu waziri wa tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Aggrey Mwanri kuingilia kati suala hilo.
“Mimi kwa kushirikiana na kamati niliyokuwa nimeiunda tumefanya jitihada za kurudisha hizo fedha ikiwa uongozi wa benki ya NMB ulikubali na hilo ni jambo la busara tumewashukuru ambapo walipiga mahesabu na kubaini kiasi cha shilingi billioni 2.1 ndizo zilizoibiwa tofauti na awali ilivyokuwa ikisemekana ni billioni 6.5 zilizoibiwa”alisema mwenyekiti Sheka.
Ikiwa alisema fedha hizo zimeelekezwa kutumika katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara za halmashauri shilingi millioni 580,maabara za vituo vya afya na zahanati shilingi millioni 200, madawati nyumba za walimu shilingi millioni 200, watendaji wa kata kununuliwa pikipiki moja kila mmoja zimetengwa shilingi millioni 40.
Pia alisema kuwa kuendeleza vikundi vidogo vidogo vya wajasiliamali na idara ya vikundi vya kilimo cha umwagiliaji jumla shilingi millioni 80,ikiwa wamefanya hivyo lengo ni kuboresha miundombinu hiyo na wananchi kuweza kunufaika na rasilimali hizo.
Aidha baadhi ya madiwani hao akiwemo Ferdnand Mpogomi wa kata ya Sekebugoro na Amani Mohamed wa kata ya Shagihili walimpongeza mwenyekiti wa halmashauri kwa jitihada alizofanya mpaka kufanikisha kurudisha kiasi hicho cha pesa,huku halmashauri ikiendelea kupata hati safi kwa miaka miwili mfululizo hilo pia la kujivunia. |
0 Response to "BENKI YA NMB TAWI LA MANONGA SHINYANGA MJINI LIMEREJESHA FEDHA HALMASHAURI YA KISHAPU."
Post a Comment