NAIBU WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI PHILIPO MULUGO.
HALMASHAURI ya Muheza mkoani Tanga
ina mpango madhubuti wa kuwachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya watu
wanaowatumikisha wanafunzi kazi mbalimbali ikiwemo ya kuchuma machungwa na
kupelekea kufanya utoro mashuleni.
Hatua hiyo imeibuka mara baada ya
afisa elimu sekondari wa halmashauri ya wilaya ya Muheza,Lusajo Gwekisa
alipokuwa akiwasilisha taarifa kwenye kikao cha baraza la madiwani iliyosema
hatua zimeanza kuchukuliwa kwa wale wote ambao wamesababisha tatizo la utoro wa
wanafunzi ambapo kesi 66 zimefunguliwa mahakamani huku wanafunzi 123 kati ya
303 wakirejeshwa masomoni.
Taarifa hiyo pia ilieleza kwamba
hali hiyo ni sehemu ya mkakati wa utekelezaji wa agizo la Rais Jakata Kikwete
ambapo ilisema kwamba kwa upande wa shule za msingi mpaka julai 27 mwaka huu
wanafunzi wapatao 170 bado walikuwa hawajaweza kurejea masomoni huku juhudi
zikiendelea.
Aidha taarifa hiyo iliendelea
kueleza kwamba mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Muheza,Ibrahimu
Matovu kwamba tayari ameshamwandikia barua hakimu mkazi mfawidhi kuhamishia
mahakama kwenye maeneo ambayo hayana mahakama za mwanzo ili kuweza
kushughulikia masuala ya mdondoko.
Wakati huo huo taarifa kutoka kwenye
kikao hicho cha madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Muheza zinaeleza msako wa
kuwanasa wale wanaowatumikisha watoto kwenye ajira zisizo rasmi unaendelea
ambapo utekelezaji ulianza tangu tarehe 8 januari mwaka huu ambapo sheria
itachukua mkondo wake.
Hata hivyo serikali imewataka
wajumbe wa baraza la madiwani hapo katika maeneo yao kuhakikisha wana wabaini
wazazi,walezi na baadhi ya wafanyabiashara wanawatumikisha wanafunzi na
kuwalipa ujira na kusababisha wimbi kubwa la idadi ya utoro ambapo ni njia
inayochangia kuwasababishia kutohudhuria masomo.
Baada ya kusomwa kwa taarifa hiyo
ndipo ilimpelekea mkuu wa wilaya hiyo,Subira Mgalu kutoa rai hiyo kwenye kikao
cha baraza la madiwani kilichofanyika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya
Muheza huku akisema ushirikiano unahitajika kutoka kwa madiwani katika kuwafichua
wamiliki wa mashamba ya machungwa sambamba na madalali ambao wamekuwa
wakiwatumia wanafunzi kwa kazi hiyo.
Alisema kwamba katika wilaya ya
Muheza kumezuka tatizo kubwa la ajira za utotoni suala ambalo limeonekana kuwa
kikwazo kwa maendeleo ya elimu ambapo vijana wengi wamekuwa wakikataa
kuhudhuria shuleni kutokana na kwenda kweye mashamba kutumikishwa wakilipwa
ujira mdogo na kuharibu maisha yao.
Mgalu alisema ili kuweza kukomesha
vitendo hivyo vinavyozorotesha maendeleo ya sekta ya elimu madiwani wanatakiwa
kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuvipatia taarifa
zitakazowezesha watu wote wanaowatumikisha wanafunzi kukamatwa na kufikishwa
mahakamani.
Akizungumzia zaidi tatizo la
mdondoko wa wanafunzi,Mgalu alisema ili kuliondosha viongozi wanapaswa
kulifanya kuwa ajenda ya kudumu kwenye vikao vyao licha ya kuwepo kwa mafanikio
ya kuanza kurejeshwa madarasani kwa baadhi ya wanafunzi waliotoroka shule
huku akisisitiza zoezi kuwa ndelevu.
|
0 Response to "HALMASHAURI YA WILAYA YA MUHEZA MKOANI TANGA IMEREJESHA WANAFUNZI 123 MASOMONI "
Post a Comment