HILI NI JENGO LA BWENI LA WASICHANA KATIKA SHULE YA SKONDARI USULE HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA.
SHULE ya sekondari
Usule iliyopo katika kijiji cha
Masekelo kata ya Bukene halmashauri ya wilaya ya Shinyanga imeanza ujenzi wa bweni la wasichana lengo ni
kupunguza utoro na mimba kwa wanafunzi wa kike ambalo ndilo limekuwa changamoto
kubwa shuleni hapo.
Ujenzi huo ambao ndio umeanza na kufikia hatua ya lenta umegaharimu
kiasi cha shilingi millioni 36
ambazo zimetolewa na halmashauri ikiwa
zinahitajika kiasi cha shilingi millioni 12 ili kuweza kukamilisha ujenzi
huo ambapo bweni hilo linatarajia
kuchukua wanafunzi zaidi ya 40 pindi litakapokamilika.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo
Paulo Maganya alisema kuwa ujenzi wa hostel utachangia kupunguza utoro
na mimba shuleni hapo kwa wanafunzi wa kike ikiwa kwa mwaka huu wanafunzi
watano walibainika kuwa na mimba,huku suala la utoro likikuwa kwa kasi kubwa kutokana na umbali mrefu kwa wanafunzi
kutembea ingawa hutumia usafiri wa baiskeli
wakati mwingine huchoka na kujikuta hawahudhurii shuleni.
“Shule hii inawanafunzi
350 ikiwa wasichana ni 200 na wavulana 150, matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka huu yalikuwa mazuri waliofaulu wasichana ni 11 na wavulana 8 na
kuifanya shule hiyo kuwa ya tatu
kiwilaya ,hivyo kama bweni la wasichana
likikamilika litaweza kudhibiti utoro na
mimba kwani wanafunzi hao wamekuwa wakitembea umbali mrefu inayowafanya kuchoka hiyo ndiyo tumeona ni
sababu mojawapo”alisema Maganya.
Naye kaimu ofisa mtendaji wa kata hiyo Edward Ndono baada ya
kuwasili mbunge wa jimbo la Solwa Ahamed Salum na kuweka jiwe la msingi katika bweni hilo alisoma taarifa juu ya shule hiyo
ambapo alieleza changamoto zinazowakabili kuwa ni uhaba wa maji, mimba kwa wanafunzi ikiwemo fedha za kukamilisha bweni hilo
sanjari na jengo la utawala lililoanza ujenzi wake tangu mwaka 2006.
Pia ofisa elimu sekondari
kutoka halmashauri hiyo Karugoba
Jesse alisema kuwa suala la mimba mashuleni limekuwa ni
changamoto kubwa ujenzi wa mabweni
utaweza kusaidia kupunguza tatizo hilo kwa kushirikiana na wazazi katika dhana
nzima ya maadili, na kila baada ya miezi
mitatu idadi ya wanafunzi watano mpaka
saba kwa halmashauri nzima wanapatikana na mimba wakiwa shuleni.
Mbunge huyo kwanza aliwataka wazazi na walezi kuwapa maadili
watoto wao na kuwaeleza madhara ya mimba za utotoni kwani wamekuwa hawatumii
hata kinga matokeo yake kupata mimba jambo ambalo ni hatari,pia suala la kukamilisha hosteli atatoa kiasi cha
shilingi millioni sita na halmashauri millioni sita ili kuweza kupatikana kiwango kinachotakiwa na ujenzi
kukamilika.
“Mimi nitatoa kiasi cha shilingi millioni sita na
halmashauri kiasi cha shilingi millioni sita
ili kuweza kukamilisha ujenzi huo, tatizo la mimba kwa wanafunzi ni
kubwa hivyo wazazi na walezi mnatakiwa
kutoa elimu ya maadili kwa watoto ili kutoweza kubeba mimba wakiwa shuleni kwa kushirikina hilo linawezekana”alisema
Mbunge Salum.
|
0 Response to "MABWENI KUPUNGUZA CHANGAMOTO YA MIMBA UTORO MASHULENI KWA WANAFUNZI WA KIKE."
Post a Comment