Habari za hivi Punde

WANAWAKE WAJITOKEZA KUPIGA KURA ZA SIRI KUBAINI WAUWAJI WA VIKONGWE.


UONGOZI WA KIKUNDI CHA SUNGUSUNGU  KATA YA ISAKA WILAYANI KAHAMA MKOANI SHINYANGA.
KATIKA kukabiliana na wimbi la mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake vikongwe wilayani Kahama mkoani Shinyanga, walinzi wa jadi Sungusungu  katika kata ya Isaka wameanzisha zoezi la upigaji wa kura za siri kwa ajili ya kuwafichua watu wanaojihusisha na mauaji hayo.

Hatua hiyo inafuatia kuzuka kwa mtindo mpya wa mauaji dhidi ya vikongwe hao ambapo hivi sasa wauaji kabla ya kutekeleza dhamira yao huwaandikia barua wanawake wanaokusudiwa kuuliwa ili wajiandae kwa ajili ya kuuawa.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika kijiji cha Mwashigina kata ya Isaka wilayani Kahama ulioitishwa na uongozi wa sungusungu, Mtemi wa sungusungu kata ya Isaka, Machimu Ndalo alisema baada ya kukithiri kwa mauaji hayo walinzi wa jadi wameamua kupigisha kura za siri katika kila kijiji ili kuwabaini wahusika.

Ndalo alisema wilaya ya Kahama inaongoza mkoani Shinyanga kwa mauaji ya vikongwe ambapo kwa kila mwezi kunaripotiwa matukio ya mauaji yasiyopungua matatu hali ambayo imewashitua wanawake wengi na kusababisha waishi maisha ya hofu kila siku kwa kutokufahamu lini watavamiwa na kushambuliwa kwa kukatwa katwa mapanga.

“Ongezeko la mauaji ya wanawake vikongwe katika wilaya yetu limetushitua sana, maana ndani ya mwezi mmoja hivi sasa vikongwe watatu wanauawa kikatili, sisi walinzi wa jadi katika kata ya Isaka tumeona tulivalie njuga suala hili, tumeamua kuendesha zoezi la upigaji wa kura za siri katika kila kijiji,tumeona tusaidiane na serikali katika vita hii,”

“Wiki iliyopita tuliendesha upigaji kura za siri katika kijiji cha Mwakata, zaidi ya wanakijiji 700 walijitokeza na kupiga kura, kura hizi hazitangazwi hadharani, baada ya kuchambuliwa na kufanyika uchunguzi wa kina tutawasilisha majina yote ya waliotajwa kwa viongozi wa serikali ili waweze kuchukuliwa hatua,” alieleza Ndalo.

Kwa upande wake Ofisa Tarafa ya Isagenhe wilayani Kahama, Kadigi Reuben aliwaomba wakazi wa kijiji cha Mwashigina kuitumia vizuri fursa hiyo kwa kuhakikisha wanawataja walengwa halisi wanaojihusisha na vitendo vya ukataji mapanga vikongwe bila ya kutanguliza chuki binafsi kwa lengo la kutaka kumkomoa mtu.

Naye Ofisa mtendaji wa kata ya Isaka Nicholaus Maya alisema matukio ya mauaji katika kata yake katika siku za hivi karibuni yamechukua sura mpya kutokana na wauaji kuamua kuwatumia mapema barua wanawake wanaokusudia kuwaua ambapo barua hizo hubandikwa katika milango ya nyumba zao wanazoishi wanawake hao.

“Hali ya mauaji kwa sasa inatisha, maana wauaji sasa wanatuma barua kwa mtu wanayetaka kumuua kabla hawajatekeleza lengo lao, tayari kuna vikongwe wawili Milembe Ngussa (70) mkazi wa Isaka na Ngolo Sakumi (69) wa kitongoji cha Kalangala waliouawa kwa mtindo huo wa kutumia barua kabla ya kufanyika mauaji,” alieleza Maya.

Baadhi ya wanawake waliozungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi la upigaji wa kura za siri katika kijiji cha Mwashigini waliiomba serikali kufanyia kazi majina yote yatakayokuwa yameongoza katika kura hizo na kwamba tabia ya kutochukuliwa kwa hatua kali dhidi ya watuhumiwa ndiyo inayochangia kuendelea kwa mauaji hayo ya kikatili wilayani Kahama.

“Tunaiomba serikali ihakikishe inatusaidia kwa kuwachukulia hatua wale wote watakaokuwa wametajwa kwa wingi katika kura hizi za siri tunazopiga kwa kata nzima, sisi wanawake ndiyo wahanga wakuu wa mauaji haya na ndiyo maana mnaona tumejitokeza kwa wingi leo hii katika mkutano huu,” alieleza Maria Mkumo mkazi wa kijiji cha Mwashigina.



0 Response to "WANAWAKE WAJITOKEZA KUPIGA KURA ZA SIRI KUBAINI WAUWAJI WA VIKONGWE."

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.