Habari za hivi Punde

MKE WA MCHUNGAJI WA KANISA LA EAGT AJIFUNGUA HIRIZI BADALA YA MTOTO.


NI maajabu ya dunia! Mke wa Mchungaji wa Kanisa la EAGT ‘Bonde la Baraka’ lililopo Kata ya Kerege Manofu, Bagamoyo mkoani Pwani, Boniface Onesmo Mahera (38) (pichani), Bentha Seth (27) baada ya kubeba mimba kwa miezi tisa  hatimaye amejifungua hirizi.

Akizungumza na waandishi wetu mwishoni mwa wiki iliyopita nyumbani kwake, mchungaji huyo alisema mbali na mkewe kujifungua hirizi, pia alitoa mawe mawili, mkaa usiotumika na kitambaa chekundu chenye ukumbwa wa ‘hendkachifu’.

NI MIMBA YA TATU KUTOKA KIMAAJABU
Akisimulia mkasa huo, mchungaji huyo alisema kuwa, awali mkewe alikuwa akipata ujauzito lakini ukifikisha miezi mitatu hutoka.“Tangu mwaka 2009 zimeshatoka mimba tatu kimaajabu. Alikuwa akishika ujauzito, ukifikisha miezi mitatu  unatoka akienda kujisaidia, hali ilikuwa mbaya sana kiasi kwamba tulikuwa tunafanya maombi kila mara na wakati huo wote mimi nilikuwa bado sijasimikwa kuwa mchungaji,” alisema mchungaji huyo.

 
Hirizi, mawe mawili, mkaa na kitambaa chekundu vinavyo daiwa kutoka tumboni mwa Bentha Seth .
 
UJAUZITO TAYARI
Akisimulia kilichotokea siku ya tukio, mchungaji huyo alisema mimba hiyo iliyozaa ‘mtoto hirizi’ iliingia Desemba mwaka jana na tangu ilipokuwa na mwezi mmoja walikuwa wakienda kliniki kupima.


“Ikiwa na mwezi mmoja tulikwenda kliniki kupima. Vipimo vilikuwa vikitoa majibu tofauti, mara hana mimba, mara mimba imetunga nje ya mfuko wa uzazi au kugoma kabisa kutoa majibu yoyote. Kwa kweli mke wangu amepitia majaribu mengi.


AOMBA NA KUFUNGA SIKU KUMI
“Basi, tukawa tunaendelea hivyohivyo huku tukiomba na kufunga kwa siku kumi kwa maombi maalum kwa mke wangu na wanawake wengine waliokuwa hawashiki ujauzito. Hatimaye tukamaliza na kusubiria mtoto atakayezaliwa,” alisema mtumishi huyo wa Mungu.

MAAJABU YAANZA
Baba mchungaji akaendelea kusema kuwa, mimba ilipofikisha miezi sita, mkewe akaanza kupata mauzauza, alianza kutokwa na haja ndogo kila wakati kama vile kuna mtu alikuwa akimmwagia maji.
“Kama hilo halitoshi kila ilipofika saa nane mchana alikuwa akichapwa viboko na mtu asiyemwona jambo lililowapa wakati mgumu zaidi.


AUZA NYUMBA, VIWANJA KUMTIBU MKEWE
Mchungaji huyo alisema baada ya kuyaona hayo aliamua kuuza mashamba na viwanja alivyokuwa navyo sanjari na nyumba aliyojenga Kigoma ili akamtibie mkewe kwa kuamini kuwa  alikuwa akisumbuliwa na Ugonjwa wa Fistula.


Alisema alimpeleka Hospitali ya Comprehensive Community Based Rehabilitation in Tanzania (CCBRT), Msasani jijini Dar ambapo vipimo vilionesha hakuwa na ugonjwa wowote, wakarudi nyumbani na kuendelea na maombi.“Nimeishapoteza karibu shilingi milioni nane kwa ajili kumtibia mke wangu na sasa hivi sina fedha tena na matatizo bado yanaendelea kuikumba ndoa yangu kila kukicha, nina imani shetani aliyeikumba nyumba yangu ataiachia kwa uwezo wa damu ya Yesu,” alisema.

SIKU YA TUKIO, SAUTI YA CHURA KWANZA
Hatimaye siku za mama mchungaji kujifungua ziliwadia, Agosti 19, mwaka huu asubuhi, mwanamke huyo alianza kwa kusikia sauti ya chura ikitokea tumboni ndipo saa tatu usiku alishikwa na uchungu huku mumewe akiwa na shilingi 1,500 tu mfukoni pesa ambayo haikuwa ikitosha hata usafiri wa kwenda hospitali.

“Nilifanya maombi mazito na kumtayarishia mkewe wangu sehemu ambayo atajifungulia hapahapa nyumbani, cha ajabu muda wa kujifungua nikashangaa kumwona anatoa haja ndogo kama ujazo wa lita kumi. Nikiwa naendelea kufanya maombi tumbo lilijaa na kupungua, ilibidi nimfunge kitambaa na mpira wa tairi la baiskeli ili tumbo lipungue.
“Kwa hatua aliyokuwa amefikia mke wangu  nilijua anaaga dunia kwa sababu niliisha kinga ndoo nne zilizokuwa zimejaa haja ndogo na hakukuwa na hata tone moja la damu.
“Ilipotimu saa sita usiku mke wangu akaanza kulalamika huku akisema anakufa, mara nikaona kitu kimechomoza, akasema nisaidie basi, nilipochungulia nikaona uzi, nikapeleka mkono kuuvuta, ikawa kama tunavutana lakini nilifanikiwa kuvuta ndiyo nikatoa hirizi lakini sikumwambia nilichokiona na muda huohuo yeye alipoteza fahamu.

“Kwa sababu ilikuwa kitu cha ajabu sana kwangu, nilitoka kwenda kuwaita majirani zangu ili waje washuhudie kilichotokea kwa mke wangu. Walikuja na kumkuta bado amepoteza fahamu.

“Alipokuja kuzinduka alianza kunidai mtoto ikabidi nimwambie ukweli mbele ya majirani. Niliichukua ile hirizi nikaifungua nikakuta ndani kuna kitambaa chekundu, mawe, mkaa na manyoya, nikaviombea na kuvichoma moto.

“Haya yote naona ni majaribu ya shetani tu na ninasema hili ni jaribu lake la mwisho haitatokea tena na kama ikitokea basi nitamteketeza huyo shetani kwa maombi,” alisema mchungaji huyo.

MAMA MCHUNGAJI SASA
Kwa upande wake, mama mchungaji huyo alisema anamshukuru Mungu kwa majaribu yote aliyopitia na kuamini ni sehemu ya maisha lakini kubwa ni uzima alionao mpaka sasa.

0 Response to "MKE WA MCHUNGAJI WA KANISA LA EAGT AJIFUNGUA HIRIZI BADALA YA MTOTO."

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.