Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu umebaini kuwa hali hiyo inaendelea katika kijiji cha Kilangawana, Kata ya Kipeta katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa ambapo imeelezwa kuwa kijiji hicho kilichopo kando ya Ziwa Rukwa na pori la Uwanda linalosemekana kuwa na tembo wanne wasiozaliana; wananchi wake mpaka sasa wanaishi kwa mashaka kutokana na vitendo wanavyofanyiwa na baadhi ya askari wa wanyamapori.
Wananchi kijini hapo wameiambia FikraPevu kuwa baadhi yao wanategemea uvuvi na biashara ya maji kutoka mto Momba na kuwa walianza kupigwa na kuporwa mali zao na askari hao mara tu baada ya ziwa hilo kufungwa tangu Desemba 31, mwaka jana kisha kufunguliwa kwa uvuvi Julai mosi mwaka huu.
Mmoja wa wanananchi hao ambaye ni mvuvi, Majuto Mwambogoja (35), amesema kuwa tangu Agosti 3, 2014, askari hao wamevamia fukwe za Ziwa Rukwa na kuanza kuwapiga wavuvi na kupora mali zao.
“Tuliamua kuandamana ili tuweze kupambana nao ili lolote litakalotokea liwe hivyo hivyo maana tunanyanyaswa, kupigwa na kuporwa mali zetu bila kutueleza tatizo letu, lakini Mwenyekiti wa CCM kata, alitutuliza na kutusikiliza lakini mambo bado yanaendelea’’ alisema Mwambogoja.
Vitisho vyatawala
Imebainika kuwa kila wakati wananchi walipowahoji askari hao ili kujua makosa yao, waliwatishia kuwa wakiendelea kutowatii watawapa kesi ya ujangili ya kukutwa hifadhini wakiwa na silaha aina ya kisu, upanga na shoka, vitu ambavyo wavuvi wanamiliki kwa ajili ya uvuvi halali.
Naye Magoma Mserikali (44) na Gwamaka Mwansasu, alikaririwa na FikraPevu akisema kama wao ni wavunjaji wa sheria walitegemea wanapokamatwa wangepelekwa mahakamani, lakini ajabu askari hao wanawapiga viboko, kupora mali zao na kuomba rushwa.
“Ilikuwa Agosti 7 na 17-18 mwaka huu, wamekuja tena wamepiga sana watu, kupora mali zikiwemo samaki, fedha, kuharibu ngalawa na kuondoka na samaki ambao wanaenda kuwauza! Tunajiuliza hii serikali ikoje wakati tunavua kihalali eneo hili? Tukikimbilia kwenye visiwa kuishi huko ndani ya maji wanatufuata nako!” alisema Mserikali.
Walisema askari hao wanafanya vitendo kama vilivyofanywa na oparesheni tokomeza, ambapo walichoma hata makazi ya watu kwa kisingizio kuwa zipo ndani ya hifadhi, jambo ambalo lilisababisha mpaka mkuu wa mkoa wa Rukwa kufika Kijijini hapo mwaka jana, na kuwa pori la Uwanda, halina ishara zozote zinazoonesha kuwa ni pori la hifadhi la serikali na kwamba wananchi hawaruhusiwi kupita ndani ya pori hilo ili kwenda kuvua samaki katika ziwa Rukwa, ingawa hakuna njia zaidi ya kupita ndani ya pori hilo.
Kijana Amon Staphod Mwandosya (25) – (Pichani), mmoja wa waathirika wa vipigo vya askari hao, ambaye mpaka sasa ana majereha ya vipigo, alisema aliitwa na askari hao kuwateremshia mzigo kwenye gari yao, baada ya hapo alihitaji kupata haki yake, akasukumwa akiwa juu ya gari, alipodondoka akaanza kushushiwa kipigo jambo ambalo lilimfanya akimbie kuokoa maisha yake.
“Ilikuwa tarehe 6 mwezi huu, niliitwa na askari hao kuwashushia mchele debe kumi kwenye gari yao, nilipomaliza na kuanza kuwadai Shilingi Elfu sita (6,000/=), ndipo wakaniambia niondoke haraka, nilipozidi kudai nikaanza kupigwa” alisema Mwandosya huku akionesha majeraha mikononi, jino lililovunjwa na kuvua nguo ili kuonesha majeraha zaidi.
Alipoulizwa kama alienda kutoa tarifa Kituo cha Polisi na kutibiwa, amesema hajaweza kufanya hivyo kwasababu hana imani kwamba angesikilizwa na mpaka sasa anaendelea kujitibu kwa kununua dawa dukani na dawa za kienyeji.
Uongozi wa Kijiji cha Kilangawana, ulipoulizwa kuhusiana na vitendo hivyo, ulisema hauna taarifa zozote za kusitishwa uvuvi, bali wanachoshuhudia ni askari hao kupita kijijini na kupiga wavuvi ziwani, ambao ni wakazi wa kijiji hicho na wengine.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Ludovick Akilimali, ameiambia FikraPevu kuwa oparesheni hiyo imezuka bila hata uongozi wa Kijiji kujua, kwasababu taarifa zilizopo ni kwamba ambao wamepigwa marufuku ni wakulima na wafugaji waliokuwa wanalima kwenye pori hilo.
Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Oscar Kamkwamba, amesema kuwa wananchi wa eneo hilo wanashindwa kuchangia maendeleo kutokana na kupigwa marufuku na askari pori kuvua samaki, kwasababu ndiyo tegemeo la uchumi wao na tayari wawakilishi wa Mkurugenzi wanayo taarifa tangu Agosti 8, mwaka huu.
“Mwenyekiti uwe unawaweka wazi waandishi wa habari, hapa Kijijini watu wote wanategemea uvuvi, hakuna hata kipande cha kulima, watu wasio wavuvi wanachota maji na kuwauzia wanaovua kwa ajili ya kunywa’’ alisema Mtendaji huo.
Kwa upande wa wajumbe wa serikali ya Kijiji ambao waliokuwepo katika mahojiano kati ya FikraPevu na Mwenyekiti wa Kijiji hicho, walisema kuwa wanaiomba serikali iangalie oparesheni hiyo na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kufika haraka eneo hilo ambapo Agosti 18, mwaka huu, yalitaka kutokea maafa makubwa baada ya askari hao kuvamia kijijini na kuanza kupora mali za watu na kuwarusha kichurachura.
Mkuu wa wilaya hiyo Mathew Sedoyeka, amekaririwa na FikraPevu akisema kuwa hafahamu kama kuna wananchi wake wananyanyaswa na kama oparesheni hiyo ni halali.
“Sina taarifa, ninachokijua ni kwamba Ziwa lilifungwa na kufunguliwa, wavuvi wameruhusiwa kuvua kuanzia Julai mosi, 2014, na watu ambao hawatakiwi kuonekana katika pori hilo ni wakulima na wafugaji siyo wavuvi kwenda kuvua” alisema Sedoyeka.
Awali wananchi hao kuwalalamikia Tanapa kuhusika na zoezi hilo ambapo FikraPevu ilipowatafuta viongozi wa Tanapa akiwemo Afisa habari wake, Pascal Shelutete, ambaye alisema kuwa pori hilo halipo chini ya TANAPA bali lipo chini ya Idara ya Wanyamapori.
Hata hivyo Ofisi ya Idara ya Wanyamapori kitengo cha habari wamesema anayepaswa kuzungumzia suala hilo ni msemaji wa Wizara ya Maliasili na utalii, Nurdin Chamuya, ambaye alipotafutwa naye alikwepa kujibu suala na kusema anayepaswa kuzungumza suala hilo ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Wanyamapori, Paul Sarakikya, ambapo juhudi za kumtafuta kwa njia ya simu, hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya kiganjani kuiba bila kupokelewa.
0 Response to "OPARESHENI TOKOMEZA UVUVI HARAMU NCHINI YAREJESHWA KINYEMELA"
Post a Comment