SERIKALI imeombwa kuangalia uwezekano wa kuwalipa kiinua mgongo wajumbe wanaounda Mabaraza ya Mamlaka ya Miji Midogo hapa nchini pindi wanapomaliza muda wao kama ilivyo kwa madiwani katika halmashauri za wilaya.
Rai hiyo ilitolewa jana na wajumbe wa Mamlaka ya Mji Mdogo katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu kwenye kikao cha baraza la mamlaka hiyo kilichofanyika mjini Nyalikungu wilayani humo.
Wajumbe hao walisema serikali imekuwa ikiwalipa madiwani kiinua mgongo pindi muda wao wa miaka mitano unapomalizika lakini kwa wajumbe wa mamlaka hizo huwa hawapewi hali ambayo hawaelewi sababu ya msingi ni ipi.
“Serikali imekuwa ikiwalipa kiinua mgongo madiwani wanapomaliza muda wao baada ya kutumikia kwa kipindi cha miaka mitano lakini kwa wajumbe wa Mamlaka za miji mdogo hakuna kitu kama hicho hapa mie nashindwa kuelewa kuna sababu ipi?’Alihoji Paschal Nkamu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Robert Mugeta, alisema utaratibu wa kuwalipa wajumbe wa Mamlaka ya Mji wanapomaliza muda wao haupo katika maelekezo ya serikali tangu hapo awali na hadi sasa hawana waraka wowote unaowaelekeza juu ya malipo hayo ya kiinua mgongo kwa wajumbe hao.
“ kulipwa au kutolipwa kiinua mgongo kwa wajumbe kunategemea waraka kutoka serikalini utaoamua na kama utawahi kuja na maelekezo muhimu basi wajumbe hao wataarifiwa mara moja lakini hadi sasa hakuna maelekezo yoyote yakuwalipa kiinua mgongo”Alisema.
Alisema kuwa kwa ufahamu wake kupitia nyaraka mbalimbali na pia amekuwa akihudhuria vikao mbalimbali vya serikali vya kujadili viinua mgongo huwa nasikia habari za wabunge na madiwani tu.
Naye Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki,Slvester Kasulumbayi(Chadema) alishauri kwa kuwa suala hilo haliko kisheria hivyo ni vizuri mchakato wakauanzisha kuanzia huku chini hadi ufike katika bunge ambacho ndicho chombo cha kutunga sheria.
‘wajumbe mimi nashauri tusichoke kupigia kelele suala hili kwani hata hizi sheria huwa zinaanzia huku chini kabla ya kufika bungeni na kutungiwa sheria sasa na sisi tuanze mchakato kwa kulipeleka suala hili serikalini kwa maandishi wakati huo naomba tuwe nasubira hadi hapo serikali itakapotoa uamuzi kuhusu malipo hayo kwani ni muhimu”alisema.. |
0 Response to "WAJUMBE WA BARALAZA LA MAMALAKA MIJI MIDOGO WAIOMBA SERIKALI KUWALIPA KIINUA MGONGO."
Post a Comment