HAPA NI NJE YA MAHAKAMA WATU WA MANISPAA YA SHINYANGA WALIVYOKUWA WAMEFURIKA
MAHAKAMA ya hakimu mkazi wa Mkoa wa Shinyanga imewahukumu
watu watano kifungo cha miaka 37 na Viboko 24 kila mmoja baada ya
kupatikana na hatia ya kuvamia na kupora Benki ya NMB tawi la Maswa kwa kutumia
silaha.
Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo Neema Gasabile aliwahukumu kifungo cha
miaka 37 na Viboko 24 kila mmoja viboko 12 wakati wa kuingia na 12 wakati wa
kutoka baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashitaka
kuwa kwa pamoja walitenda kosa hilo kinyume cha sheria.
Washitakiwa hao ni Kapama Hamis Ramadhan (37), Mussa Athuman Buberwa (38), Amos
Mathayo, Lucas Vicent Mabela (40)na Zainabu Mchau (60) wote kwa pamoja
walipatikana na hatia ya makosa tisa ya jinai.
Mbele ya Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo, Mwendesha mashitaka Mwanasheria
wa Serikali Edith Tuka aliieleza Mahakama hiyo kuwa washitakiwa wote kwa
pamoja walitenda kosa hilo majira ya saa 6:00 mchana Julai 5, mwaka 2010 mjini
Maswa.
Akifafanua mashitaka hayo Tuka alisema kuwa mara baada ya kuvamia ndani ya
benki hiyo washitakiwa waliwashambulia askari wa Polisi kwa Silaha na
kuwajeruhi kwa kipigo baadhi ya wafanyakazi na wateja wa benki hiyo.
“Mbali na Vitendo vya kuwashambulia na kuwajeruhi Askari wa polisi, Wafanyakazi
na baadhi ya wateja wa benki hiyo lakini pia watuhumiwa waliteka gari aina ya
Land rover 109 iliyotumika katika uvamizi huo kisha wakapora fedha taslimu na
mali nyingine ambayo thamani yake bado haijajulikana” alisema
Mwendesha mashitakaTuka.
Akifafanua kuhusu mashitaka yaliokuwa yanawakabili washitakiwa hao kabla ya
kifungo hicho Tuka alisema ni pamoja na kufanya uporaji wa kutumia
nguvu na silaha, kumiliki silaha bila kibali cha serikali, kujeruhi, kuteka
gari na kupora mali na fedha katika siku na muda uliotajwa mjini Maswa.
Kwa upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi 24 na vielelezo mbalimbali
ikiwamo Vipimo vya Vinasaba (DNA) Vilivyowahusisha watuhumiwa
na tukio hilo.
Awali Mwendesha mashitaka huyo aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa
washitakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaotenda makosa kama hayo kwa
kuwa hivi sasa vitendo hivyo vimeshamiri nchini.
Mamia ya wakazi wa Mkoa wa Shinyanga walifurika ndani na nje ya Mahakama hiyo
iliyokuwa chini ya ulinzi mkali wa askari Polisi na Magereza kushuhudia
hukumu yenye kurasa 200 iliyosomwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo aliyoisoma
kwa takriban saa tatu. |
0 Response to "WATU WATANO WAHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 37 KWA WIZI WA BENK YA NMB- WILAYANI MASWA"
Post a Comment