Habari za hivi Punde

WATOTO WAUA BABA YAO KWA KUMPIGA FIMBO

Polisi Wilaya ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera wanawashikilia watoto watatu wa Kijiji cha Mkunyu, Kata ya Kikukuru wilayani Kyerwa mkoani Kagera kwa tuhuma za kumuua baba yao, Henry Siliakus (62) kutokana na mgogoro wa kifamilia.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Gilles Muroto alisema mauaji hayo yalifanyika Jumatatu wiki hii kijijini hapo.
“Uchunguzi wetu wa awali unaonyesha kulikuwa na ugomvi wa kifamilia, watoto walikuwa wanamlalamikia baba yao kwa kuuza chakula na kusababisha kukumbwa na njaa. Lakini kama hiyo haitoshi, baba yao alikuwa akitumia vibaya fedha hizo,” alisema Muroto na kuongeza;
“Wakati wa ugomvi huo, watoto walimshambulia baba yao kwa fimbo. Walimpiga kichwani na kusababisha kifo chake, tunasubiri taarifa ya daktari ili kujua aina ya kesi wanayotakiwa kufunguliwa na bado tunaendelea na upelelezi kabla ya kuwafikisha mahakamani.”
Alisema kuwa mmoja wa watoto hao anasoma kidato cha pili katika Sekondari ya Mkunyu, wengine wawili wanasoma Shule ya Msingi Mkunyu.
via>>Mwananchi
KARENY. Powered by Blogger.