WANANCHI wa Kata ya Chakwale Wilaya ya Gairo mkoani hapa, wamechoma
moto na kuteketea kabisa, Ofisi ya Ofisa Mtendaji wakimtuhumu kuhusika
na ubadhirifu wa fedha, kuwanyanyasa na kuwaweka ndani pindi
wanapofuatilia michango mbalimbali ya maendeleo.
Baadhi ya wakazi wa Chakwale waliohojiwa kwa
nyakati tofauti baada ya tukio hilo, walisema wananchi hao walichukua
uamuzi huo kwa jazba, kutokana na manyanyaso ya muda mrefu yaliyokuwa
yakifanywa na Mtendaji Hamza Mbalale, ambaye amekuwa akitumia mabavu
kuwaongoza kwa mgongo wa kulindwa na baadhi ya viongozi wa juu
serikalini katika Wilaya hiyo.
Kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wananchi hao walisema Mtendaji
huyo alikuwa akidiriki kuwafuata wananchi wakiwa kwenye majukumu yao
yakiwemo ya kazi na kuwakamata na kuwaweka ndani, akiwalazimisha kutoa
michango ya shule, mambo ambayo wanaamini yangeweza kufanyika kwa
mazungumzo na ushawishi.
Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu, Mtendaji huyo alisema tukio
hilo la kuchomwa moto kwa ofisi hiyo lilitokea mwishoni mwa mwezi
uliopita majira ya usiku, muda mchache baada ya kuwa amekwenda polisi
kutoa taarifa za fujo zilizoanza kujitokeza baada ya kuwekwa ndani kwa
watu walioshindwa kuchangia michango ya maendeleo ya kata.
Alisema, kikubwa wananchi wa Kijiji cha Chakwale wamekuwa na usumbufu
mkubwa wa kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo, ambako kwa
mujibu wa maazimio ya mikutano mikuu ya vijiji, ilimriwa kila mwananchi
mwenye miaka 18 hadi 60, alipaswa kuchangia sh 5,000 kwa mradi mmoja
wa maendeleo.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Hanifa Karamagi, hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo baada ya simu yake kuita bila kupokewa.
0 Response to "WANANCHI GAIRO WACHOMA MOTO OFISI YA MTENDAJI WA KATA."
Post a Comment