VITUO vya kutolea huduma
kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi mkoani Shinyanga vinakabiliwa na
changamoto ya upungufu wa mashine za kupimia CD4 hali inayosababisha hofu
kwa watumiaji wa dawa za kufubaza makali (ARV).
Hayo yalisemwa jana na
watoa huduma ya elimu ya VVU na UKIMWI ngazi ya jamii wakati wa warsha ya siku
3 iliyofanyika mjini Kahama iliyoandaliwa na Shirika lisilo la
kiserikali la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI)
linalojihusisha na mapambano dhidi ya VVU na ukimwi.
Watoa huduma hao
walisema mashine za kupimia CD4 katika Vituo vingi vya kutolea huduma
vimekuwa vikiharibika mara kwa mara hali inayosababisha watumiaji washindwe
kuelewa maendeleo ya afya zao kwa kuchelewa kupata huduma.
Mmoja wa washiriki wa
warsha hiyo Vedastus Mtange kutoka manispaa ya Shinyanga alisema kutokana na
kukosekana kwa mashine hizo wanashindwa kubaini kuwa CD4 za mgonjwa zimepanda
au zimeshuka hivyo kuiomba serikali kutatua changamoto hiyo haraka ili kuokoa
maisha ya watanzania.
“Kuna changamoto ya
mashine za kupimia CD4 katika vituo vingi vya kutolea huduma kwa watu
wanaoishi na Virusi vya Ukimwi ,wanapokosa huduma ya vipimo wengine wanaamua
kuacha kutumia dawa na kutohudhuria kliniki matokeo yake afya zao
zinadhoofika”,alieleza Mtange.
“ Changamoto nyingine ni
watumiaji wa dawa za kufubaza makali ya VVU kutokuwa na anuani sahihi kwani
wengine wamekuwa wakiandikisha majina tofauti na yale wanayotumia kwenye maeneo
wanayaoshi,hali inayosababisha ugumu katika kufuatilia maendeleo ya afya
zao”,aliongeza Mtange.
Afisa Miradi Huduma
Unganishi kwa jamii kutoka Shirika la AGPAHI,Secilia Yona alisema lengo la
warsha hiyo ni kuwajengea uwezo watoa huduma ya elimu ya VVU na UKIMWI ngazi ya
jamii ili waweze kuwaunganisha
wateja kutoka kwenye ngazi ya jamii kwenda kwenye vituo vya afya.
Akizungumza na mwandishi wa habari
Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt
Ntuli Kapologwe alisema kuharibika kwa mashine hizo kunatokana utunzaji
kutokuwa mzuri katika vituo sambamba na baadhi ya watoa huduma katika vituo
kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya mashine hizo.
Dkt Kapologwe alisema pia wanaendelea kutoa elimu kupitia kwa
viongozi wa dini,waganga wa tiba za asili na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa
wateja walioanza kutumia dawa kuhudhuria kliniki mara kwa mara ili kujua
maendeleo ya afya zao.
Hata hivyo alisema bado
kuna changamoto kwa baadhi ya wananchi kuamini katika imani za kishirikina
kwamba hajaambukizwa VVU hivyo wanaacha tiba waliyoanza na kukimbilia kwa
waganga wa jadi kitendo ambacho alisema kinasababisha baadhi ya wateja kupotea
katika huduma.
|
0 Response to "KUKOSEKANA KWA MASHINE ZA CD4 ZAWATESA WENYE MAAMBUKIZI YA VVU."
Post a Comment