Habari za hivi Punde

MTOTO ANUSURIKA KUCHINJWA NA BABA YAKE MZAZI KISA KUCHOKA KUMTIBU MARADHI YANAYOMSUMBUA.



MWANAFUNZI  wa darasa la tatu katika shule ya msingi Majengo wilayani Kahama mkoani Shinyanga Said Joshua (12) amenusurika kufa baada ya kutaka  kuchinjwa kwa kutumia kisu na baba yake mzazi kutokana na kile kinachodaiwa kuchoshwa kumtibu kwa   maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.
Tukio hilo limetokea jana saa 11 alfajiri katika kijiji cha Majengo ,kata ya Majengo,tarafa ya Kahama mjini ambapo mwanamme aitwaye Joshua Salvatory(37) mkazi wa Majengo,fundi baiskeli akiwa nyumbani kwake alimkata kisu shingoni mtoto huyo na kuathiri koromeo lake.


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya KahamaDkt Joseph Fwoma alisema mtoto huyo alifikishwa hospitalini hapo baada ya kuokotwa na wasamaria wema huku akivuja damu nyingi shingoni.

Dkt Fwoma alisema baada ya mtoto huyo kufikishwa hospitalini madaktari walimfanyia upasuaji na kumshona sehemu ya koromeo aliyochinjwa na hali yake inaendelea vizuri hasa baada ya kuongezwa damu.

Kwa mujibu wa mama mzazi wa mtoto huyo Mariamu Idd (35) alisema, mtoto wake alichukuliwa na baba yake mzazi siku moja kabla ya tukio na  kwenda naye kwake mitaa ya Majengo kwa kuwa  alikwisha achana na mwanamme huyo siku nyingi.

“Leo asubuhi nimepigiwa simu na kuelezwa taarifa za kuchinjwa kwa mwanangu na baba yake mzazi na baada ya tukio hilo amekimbilia kituo cha polisi Mjini Kahama kwa lengo lakujisalimisha na hadi sasa ameshikiliwa huko”,alieleza mama wa mtoto huyo.

“Baba wa mtoto huyu siku za nyuma,alikuwa akimchukua mwanangu mara kwa mara na kumpeleka nyumbani kwake,mimi nilishaachana naye, huwa anamrudisha,na amekuwa akidai kuchoshwa na huduma za matibabu kutokana na mtoto huyo kuwa na matatizo ya kiafya”,alifafanua mama huyo.

Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limethibitisha kutokea kwa tukio hilo,ambapo,kamanda wa  polisi mkoa wa Shinyanga  Evarist Mangalla alisema chanzo cha tukio hilo kinasadikiwa kuwa mtuhumiwa anaugua ugonjwa wa akili.

Wakati huo huo mtoto wa kiume (miezi 6) asiyefahamika jina wala makazi yake amekutwa kichakani akiwa amefariki dunia na mwili wake ukiwa hauna jeraha na ukiwa tayari umeanza kuharibika.

  Kamanda alisema tukio hilo lilitokea Machi 4,mwaka huu saa 12 jioni katika kijiji na kata ya Mhongolo wilayani Kahama na kuongeza kuwa inaonesha mtoto huyo alitupwa katika siku tatu zilizopita huku  chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa.

0 Response to "MTOTO ANUSURIKA KUCHINJWA NA BABA YAKE MZAZI KISA KUCHOKA KUMTIBU MARADHI YANAYOMSUMBUA."

Post a Comment

KARENY. Powered by Blogger.